Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
IKIWA ni siku ya 42 tangu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alipopigwa risasi Septemba 7 mjini Dodoma, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ameeleza mambo 12 makubwa juu ya mwanasheria huyo nguli.
Hali ya afya ya mwanasiasa huyo sasa inatajwa kuwa imeimarika kiasi cha kuondolewa mashine zote zilizokuwa zinamsaidia kuishi akiwa chumba cha wagongwa mahututi (ICU), kiasi cha kuanza kula mwenyewe.
Kwa mujibu wa Mbowe, kutokana na maendeleo hayo makubwa hivi karibuni Lissu atazungumza na Watanzania kutokea jijini Nairobi, nchini Kenya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mbowe alisema hali ya Lissu imendelea kuimarika na wakati wowote kuanzia sasa ataruhusiwa kutoka wodini.
Mbowe alisema baada ya awamu ya kwanza ya matibabu yaliyofanyika mjini Dodoma na ile ya pili inayoendelea Nairobi, sasa anatarajiwa kuendelea na matibabu mengine ya awamu ya tatu nje ya Afrika.
“Hadi sasa Lissu amefanyiwa upasuaji mara 17, amewekewa damu nyingi kuliko mgonjwa yeyote aliyewahi kutibiwa katika hospitali ya Nairobi kwa miaka 20.
“Wiki iliyopita alitoka hospitali na mashine zote zilizokuwa zinamsaidia kuimarisha afya yake ikiwemo ya figo imeondolewa na sasa hivi hatumii tena oksijeni wala mirija ya chakula. Kwa sasa anakula mwenyewe.
“Juzi (Jumapili) kwa mara ya kwanza alikaa, viungo vyote vimeshaungwa japo itahitajika miezi kadhaa kukaa sawa. Na wiki hii kwa mara ya kwanza ameliona jua, ni miujiza na imeendelea kuwa miujiza. Ni jambo la kumshukuru sana Mungu.
“Tunawashukuru madaktari wote kuanzia wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na jopo la madaktari 12 lililokuwa likimuhudumia Lissu katika Hositali ya Nairobi. Walipigana usiku na mchana kuokoa maisha yake,” alisema.
Mbowe alisema Lissu amemaliza awamu ya pili ya matibabu na kwamba kabla ya mwisho wa mwezi huu ataruhusiwa kutoka wodini.
“Lissu ameshaimarika vya kutosha na anajitambua vizuri na kwa mwezi mmoja na nusu tulikataa kutoa picha zake lakini kuanzia leo (jana) tutaanza kuzitoa ili kuwatia moyo Watanzania na mtamsikia kwa sauti na kuiona video yake.
“Tuna uhakika Lissu atarudi barabarani atafanya kazi zake na Watanzania wataendelea kufaidi matunda yake,” alisema.
AWAMU YA TATU YA MATIBABU
Mbowe alisema baada ya kutoka wodini Lissu atapelekwa katika nchi nyingine kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
Hata hivyo hakuwa tayari kutaja nchi hiyo kwa kile alichodai kuwa ni sababu za kiusalama.
“Awamu ya tatu ya matibabu itafanyika nje ya Nairobi na kwa sababu za kiusalama hatutaeleza anakwenda wapi, wakati mwafaka ukifika mtaambiwa.
“Focus (kipaumbele) yetu kama chama ilikuwa kumtoa katika hatari na kumrejesha katika uzima, hivyo suala la ulinzi wake litaendelea kuwa kipaumbele kikubwa,” alisema Mbowe.
GHARAMA ZA MATIBABU
Mbowe alisema hadi sasa gharama za matibabu zilizotumika ikiwa ni pamoja na kulipa jopo la madaktari 12 linalomuhudumia Lissu ni Sh milioni 412.4.
Hata hivyo gharama hizo hazihusishi malazi, chakula wala matumizi mengine madogo madogo.
Alisema kati ya gharama hizo, Sh milioni 280 ni fedha zilizopatikana kupitia michango mbalimbali na kwamba kila pengo linalojitokeza linazibwa na chama chake.
“Japo gharama ni kubwa lakini si kubwa kama maisha ya Lissu, michango iliyotolewa imewezesha kwa kiwango kikubwa kusaidia matibabu yake.
“Watanzania, viongozi wa chama, familia, wabunge wote, wafanyabiashara wadogo na wa kati, Watanzania waishio nje, Mange Kimambi, Wema Sepetu na wengine wengi walifanya kazi kubwa sana.
“Tunaomba Watanzania wasituchoke, waendelee kumpigania Lissu kwa sababu bado zinahitajika fedha nyingi,” alisema Mbowe.
Kwa mujibu wa Mbowe, kati ya michango hiyo fedha zilizochangwa kupitia akaunti maalumu ya chama iliyoko katika Benki ya CRDB ni Sh milioni 98, wabunge wa Chadema (Sh milioni 48.4), posho za wabunge wote (Sh milioni 43), Watanzania waishio nje (Diaspora – dola za Marekani 29,700), wananchi na viongozi wa chama (Sh milioni 24.4) na wafanyabiashara wadogo na wa kati waliochangishwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Sh milioni 28).
Alisema pia mazungumzo yalifanyika baina ya familia na Bunge kuhusu haki na stahiki za Lissu lakini akasisitiza kwamba kipaumbele chao si fedha bali kumsaidia mgonjwa apone.
“Hili jambo lina siasa na hisia kali ndani yake, si kwamba hatutaki fedha ama tuna fedha, lakini sisi kama chama tutapigania wajibu wetu wa msingi, tunasema ni bora ‘tu-struggle’.
“Misimamo ya chama chetu haitayumbishwa na fedha zozote zile, tunajali dignity (utu),” alisema.
Camera za CCTV
Alisema kamera za CCTV zilizokuwa zimefungwa jirani na nyumba ya Lissu, ambazo zinaaminika kuwa zilirekodi tukio zima la mbunge huyo kushambuliwa, kwa sasa zimeondolewa.
Alisema kamera hizo zilikuwa zimefungwa katika nyumba ya waziri mmoja iliyo jirani na nyumba ya Lissu katika eneo la Area D mkoani Dodoma.
Mbowe alisema walibaini kuondolewa kwa kamera hizo kupitia vyanzo vyao vya kiuchunguzi.
“Suala la ulinzi na usalama kwa Lissu si jambo dogo, taarifa zetu za kiuchunguzi zinaonyesha kwamba CCTV iliyokuwa imefungwa kwenye nyumba ya waziri jirani na nyumba ya Lissu imeondolewa.
“Sasa zimeondolewa na nani na kwa sababu zipi, sisi hatuko hapa kumtaja kwa sababu si mamlaka ya uchunguzi,” alisema Mbowe.
Alisema wanaamini waliomdhuru Lissu wapo na wanajulikana kwa sababu shambulio hilo lilifanyika mchana katika makazi ya viongozi.
“Shambulio dhidi ya Lissu lilifanyika mchana katika makazi ya viongozi ambako kuna kamera za kuchukua matukio yote.
“Polisi walifika eneo la tukio baada ya saa 2 tangu Lissu ashambuliwe, kwanini tusiingiwe hofu kwamba ulikuwa ni mkakati wa makusudi kuwatoa washambulizi?” alihoji Mbowe.
DEREVA WA LISSU
Mbowe alisema chama chake hakijamficha dereva wa Lissu na wala si kazi yao kumleta na kwamba polisi wakiamua wanaouwezo wa kwenda kumchukua na kuendelea naye.
“Hatuna mamlaka ya kumtoa dereva, Lissu alikusudiwa kuuawa na kiuhalisia hata dereva alikusudiwa kuuawa,” alisema Mbowe.
FAMILIA YA LISSU
Mbowe alisema kwa sasa wataiachia familia ya Lissu kufanya maamuzi ya ndani na kueleza maendeleo ya afya ya mbunge huyo .
“Kwa kipindi chote familia ya Lissu imekuwa na msimamo kama yeye mwenyewe alivyo na ina madaraka makubwa kwa mgonjwa kuliko sisi wana jamii wengine.
“Tulijipa jukumu la kumsemea Lissu akiwa mahututi lakini kwa sasa tutakasimu mamlaka kwa familia kwa sababu ameshaimarika vya kutosha na anajitambua vizuri.
“Lakini hatuwezi kujivua wajibu, tutaendelea kuwajibika nyuma ya familia kwa hatua zozote…hatutaki tuingie mpaka uvunguni,” alisema Mbowe.
WAPELELEZI HURU
Chama hicho kimeendelea kusisitiza juu ya kuwapo kwa wachunguzi huru kutoka nje ya nchi kwa madai kuwa hawana imani na vyombo vya dola.
“Tumeumizwa mara nyingi, watu wetu wamepotea, wengine wameuawa na hakuna hata siku moja vyombo vyetu vilituletea aliyehusika. Je, mnategemea sisi tuna moyo wa chuma?” alihoji Mbowe.
Alisema vyombo vya dola vya ndani si kwamba havina uwezo lakini ili haki itendeke na kuonekana imetendeka wanataka jambo hilo lipewe kipaumbele na vyombo vya nje kwa sababu viko tayari lakini serikali ndio imekuwa kikwazo.
“Si mara ya kwanza watu kutoka nje kuja kufanya uchunguzi nchini, Scotland Yard walichunguza moto uliotokea katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1984, hivyo IGP Sirro na Mwigulu (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), wasiogope kama wanajiamini waruhusu wachunguzi huru waje,” alisema.
HOFU DHIDI YA VIONGOZI
Chama hicho kimesema kinazo taarifa juu ya kuwapo kwa mipango ya kuwadhuru viongozi wengine lakini hakitarudi nyuma.
“Kuna ambao tunaitwa viherehere kutokana na kumpigania Lissu, tunajua nini kinapangwa lakini hatutarudi nyuma.
“Hatutamuogopa yeyote, tutaukataa umauti kwa nguvu zote za sala na mikakati yoyote ile, tutapigania haki, ukweli na ustawi wa taifa letu,” alisema Mbowe.
LISSU ALIVYOSHAMBULIWA
Septemba 7 mwaka huu, Lissu alishambuliwa kwa risasi wakati akirejea nyumbani kwake Area D mkoani Dodoma baada ya kutoka kuhudhuria vikao vya Bunge.
Baada ya shambulio hilo alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na baadaye kusafirishwa kwa ndege kwenda Nairobi, Kenya ambako anaendelea na matibabu.