Na Jeremia Ernest, Mtanzania Digital
Mbunifu nguli wa mavazi nchini, Mustafa Hassanali, amekonga nyoyo za wadau wa tasnia ya mitindo kupitia Collection yake mpya ya ‘Royal Tour‘ katika onyesho la ubunifu wa mavazi lililokuwa na lengo la safari mkoani Manyara.
Akizungumza na Mtanzania Digital, Hassanali amesema lengo la jukwaa hilo la mavazi ni kushawishi watalii kununua nguo zao za safari hapa Tanzania hatua ambayo itasaidia kutangaza na kukuza sekta ya utalii nchini.
Onyesho hilo limefanyika leo Jumamosi Januari 29, 2022 katika Hoteli ya Mawemawe, na kuhudhuriwa na wabunifu, wanamitindo na wadau wa mitindo kutoka pande nne za dunia.
Hassanali amesema yupo tayari kutumia kipaji chake kwa ajili ya manufaa ya nchi nakwamba ndiyo sababu ya kuvunja ukinya wa miaka mitatu ambao amekuwa nao katika tasnia hiyo.
“Rais wetu Mama Samia Suluhu Hasani, amefungua njia kwa kutuonyesha fursa katika sekta ya utalii na mimi kama mbunifu ambaye sijatambulisha mavazi yangu takribani miaka mitatu,hivyo leo nimevunja ukimya huo kwa kutoa ushirikiano katika kufanikisha kutangaza nchi na kuhamasisha ubunifu wa nguo za safari kwenye sekta ya utalii,” amesema Hassanali.
Ameongeza kuwa anaishukuru Wizara ya Maliasili na Utaliipamoja na Viongozi wa mikoa ya Manyara na Arusha na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Ngorongoro Conservation kwa kutunza na kuenzi mbuga.
Asante