MBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (CCM), amezindua tovuti ya Jimbo la Musoma Vijijini ili wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wapate taarifa mbalimbali kuhusu jimbo hilo.
Uzinduzi wa tovuti hiyo ulifanyika katika Kijiji cha Saragana, wilayani Musoma ambapo wananchi na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Musoma Vijijini walihudhuria.
“Badala ya kusubiri kuangalia runinga au magazeti, tovuti hii itasaidia shughuli mbalimbali za jimbo ikiwamo miradi mbalimbali tunayotekeleza kuonekana duniani.
“Tovuti hiyo itarahisisha mawasiliano kati ya mbunge na wananchi kwani sasa wataweza kuuliza maswali au kutoa maoni yao moja kwa moja kuhusu jimbo lao.
“Kuonekana kwa miradi inayotekelezwa jimboni hapa ikiwamo miradi ya afya, elimu na kilimo, kutasaidia kuvutia wafadhili mbalimbali kuendeleza miradi husika,” alisema Profesa Muhongo ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini.
Katika maelezo yake, Profesa Muhongo alisema uchangiaji wa fedha za kutengeneza madawati unaoendelea sasa jimboni humo utawezesha madawati 8,000 kutengenezwa.
Pamoja na hayo, awali Profesa Muhongo alizindua pia mpango wa ugawaji madawati jimboni kwake ambapo alizindulia mpango huo katika Shule ya Msingi Rukuba, iliyopo katika Kisiwa cha Rukuba ambayo ilipata madawati 100.
“Jimbo letu lina upungufu wa madawati 8,000, hivyo utengenezaji wa madawati haya unaendelea kupitia Suma-JKT mkoani Mwanza na fedha za kutengenezea madawati nimezitoa mimi kupitia kwa wadau mbalimbali walioguswa na tatizo hilo.