29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

MUHIMBILI, MOI HOI KWA KUKOSA FEDHA ZA MAENDELEO

Na VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, imeshangazwa na kitendo cha serikali kutozipatia fedha za miradi ya maendeleo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kama walivyoomba na kuidhinishwa na Bunge.

Katika mwaka wa fedha 2016/17, Muhimbili iliomba kiasi cha Sh bilioni 4 na MOI iliomba kupatiwa Sh bilioni 4.8, lakini fedha hizo hawajapatiwa hadi hivi sasa.

Yalibainika hayo jana wakati kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Peter Serukamba ilipofanya ziara katika hospitali hizo.

Kutokana na hali hiyo, wajumbe walimbana kwa maswali Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangwalla wakimtaka aeleze sababu za Serikali kutotoa fedha hizo.

Hoja hiyo iliibuka baada ya Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru kueleza kwamba hawajapokea fedha hizo walizoomba.

“Tuliomba Sh bilioni 4, hatukupewa fedha yoyote, katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2016 tulipokea misaada ya thamani ya Sh milioni 218.044 kutoka kwa wahisani, na tulipokea mkopo wa Sh bilioni 7.897 kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),” alisema.

Alisema fedha hizo walizitumia kununua vifaa tiba ikiwamo Ct-Scan na ukarabati wa wodi na vyumba vya upasuaji.

Profesa Museru alisema kwa kuwa hospitali hiyo ina muda mrefu tangu imejengwa, inahitaji ukarabati mkubwa na ununuzi wa vifaa tiba kwani vilivyopo vimechakaa na vingi vimeharibika.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema jambo hilo linashangaza kwani wabunge wanapopitisha bajeti, Serikali inakuwa imeelezwa nini cha kufanya.

“Kila mwaka tunapitisha bajeti, lakini kila tunapopita tunaambiwa fedha za maendeleo hazijapelekwa, kwanini hazipelekwi wakati zilipitishwa?” alihoji.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema), alisema ni muhimu Serikali ikawa makini katika suala hilo na kwamba bajeti inapopitishwa ipelekwe kwa wakati.

Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndungulile (CCM), alisema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kutengeneza vifaa tiba, hivyo wakati umefika ikashirikiana na watu wengine kwa kuwaruhusu kuwekeza vifaa tiba na hospitali zake zibaki kutoa tiba.

Akijibu hoja hizo, Dk. Kigwangwalla alikiri kuwapo changamoto ya fedha inayozikabili hospitali hizo, hata hivyo alisema zinafanyiwa kazi na Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles