Aveline kitomary
Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema hospitali hiyo itaanza kupandikiza figo kwa wagonjwa walioko katika hali hatarishi ‘high risk’ kama wagonjwa wenye maambukizi ya VVU na Homa ya ini.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya figo Duniani, amesema uwezo wa wataalamu katika hospitali hiyo wa kupandikiza figo umefikia asilimia 100 hivyo kuanzia mwezi Aprili wataalamu wao hawatahitaji msaada kutoka nje.
“Mpaka sasa jumla ya wagonjwa 56 wameshafanyiwa upandkizaji wa figo katika hospitali hii na kwa nchi nzima wagonjwa 1000 wamepata huduma ya uchujaji damu kati ya hao Muhimbili ni 350 na Mloganzila ni 70,”ameeleza Prof Museru.
Amesema kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa jengo la upandikizaji viungo katika Hospitali ya Mloganzila ambapo jengo hilo litakapokamilika jumla ya wagonjwa wawili hadi watatu watapandikizwa figo kwa siku moja sawa na wagonjwa 200 hadi 300 kwa mwaka.