32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MUGABE KAONDOKA NA REKODI YA KUWANANGA BUSH, BROWN

Na, ALOYCE NDELEIO


LICHA ya kufikia ukomo wa utawala wake uliodumu kwa miaka 37 kwa namna ambayo sivyo ingestahili kwa kiongozi aliyeshiriki katika ukombozi wa nchi yake hawezi kukosa jambo ambalo linaonesha ujasiri wake katika kupinga mambo ya ukandamizaji kutoka nchi za Magharibi.

Hivyo ndivyo alivyokuwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na alilidhihirisha hilo wakati wa utawala wake dhidi ya Rais George Bush wa Marekani ambaye alimweleza kuwa anaua watu wasio na hatia huko Irak na Afghanistan hivyo Serikali yake haina uhalali wowote wa kujifanya ni msimamizi wa Haki za Binadamu popote duniani.

Alikuwa akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, alisema, “Jana (Jumanne Septemba 25, 2007) mmesikia Bwana Bush hapa akiita Serikali yangu ‘Utawala wa Mugabe’. Ninaitwa dikteta kwa sababu nimekataa fikra hasi kandamizi (kwamba nchi za Magharibi zina haki juu ya rasilimali za Zimbabwe) ana kukatisha tamaa wakoloni-mamboleo.”

Aliongeza kwamba Rais Bush, Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Tony Blair na aliyemfuatia, Brown wanaamini rasilimali za Zimbabwe zinastahili kumilikiwa na jamaa na rafiki jambo ambalo Zimbabwe inalikataa.

“Nchi za Magharibi bado zinazuia uhuru wetu kwa njia ya umiliki wa rasilimali na katika mchakato huo tumegeuzwa kama bidhaa katika ardhi yetu. Katika nchi yangu na nchi jirani yetu kitu kikubwa wanachotumia sasa ni ardhi waliyotunyang’anya wakati wa ukoloni wa Waingereza.

“Uthibiti huo bado unaendelea, ingawa unapingwa kwa nguvu zote nchini Zimbabwe na hivyo kuchochea mgogoro uliopo hivi sasa baina yetu na Uingereza inayosaidiwa na maswahiba zake hususani Marekani na Australia.”
Rais Mugabe alisema kuwa Zimbabwe ilipata uhuru wake baada ya mapambano na ukoloni wa Waingereza, uliokuwa unasaidiwa na nchi za Magharibi ambazo ndio za kwanza kutia sahihi tamko la dunia la Haki za Binadamu mwaka 1948 maarufu kama Universal Declaration of Human Rights kwa Kiingereza.

Rais Mugabe alisema hata baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945, nchi za Magharibi ziliona kwamba uamuzi wa awali wa mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 ya kugawa Afrika vipande vipande ili kunyonya Waafrika bado yalikuwa na nguvu kuliko tamko la dunia la Haki za Binadamu. Wakati huo tamko la Haki za Binadamu halikuwa na maana kwa haki za Waafrika mbele ya maslahi ya kiuchumi na ubaguzi wa rangi.

“Namtaka Bwana Bush asome historia vizuri. Namtaka atambue kwamba yeye binafsi na kama Rais wa Marekani anasimamia ‘ustaarabu’ uliovamia nchi za watu, kuzigeuza makoloni, kudhalilisha na kuua watu. Ana mengi ya kujifunza na kidogo sana cha kutuhubiria kuhusu tamko la Dunia la Haki za Binadamu. Mikono yake inachuruzika damu za watu wa mataifa mengi
“Bado anaua. Anaua huko Irak. Anaua huko Afghanistan. Huyo ndiye anataka tumfanye kiongozi wetu kuhusu utekelezaji Haki za Binadamu? Anafunga watu. Anafunga watu na kutesa huko Guantanamo. Anafunga watu na kutesa huko Abu Ghraib. Ana magereza ya siri ya kutesa watu huko Ulaya.

“Ndiyo, hata hapa Marekani anafunga watu na magereza yamejaa watu weusi ambao idadi yao ni kubwa kushinda wanafunzi wote wa vyuo vikuu. Hata wakati mmoja alitupa kabisa hilo tamko la dunia la Haki za Binadamu. Angalia Guantanamo kwa mfano, hakuna sheria ya kimataifa inayotumika pale.

“Pale sheria za Marekani na mataifa mengine hazifanyi kazi. Ni sheria za Bush tu ndio zinatumika pale. Je,Jumuiya ya Kimataifa inaweza kukubali kusikiliza mtu huyo akihutubia kwa kigezo cha tamko la Dunia la Haki za Binadamu? Bila shaka haiwezekani,” alisema Rais Mugabe huku akishangiliwa kwa nguvu na ukumbi mzima uliojaa viongozi waliokuwa wanamsikiliza.

Rais Mugabe alifananisha rekodi za haki za binadamu za Rais Bush na jinsi Zimbabwe ilivyowatendea wakoloni wake wa zamani walioua maelfu ya Wazimbabwe wasio na hatia wakati wa vita vya ukombozi dhidi ya utawala wa Rhodesia. Alisema wakoloni hao katili hawakufungwa wala kuteswa baada ya Zimbabwe kupata uhuru wake mwaka 1980 na matokeo yake ni Rais Mugabe kupendekezwa kupewa nishani ya Kimataifa iitwayo Nobel Peace Prize.

Rais Mugabe alikumbushia kifungo chake cha miaka 11 wakati wa utawala wa Rhodesia chini ya Waziri Mkuu Ian Smith na miaka 15 aliyotumikia vita vya ukombozi dhidi ya utawala uliokuwa unasaidiwa na nchi za Magharibi zinazomtuhumu leo.
“Nimetumikia miaka 11 gerezani chini ya utawala wa mtu mweupe ambaye nimeheshimu na kulinda uhuru wake toka siku ya kwanza ya uhuru wa Zimbabwe, naye si mwingine bali ni Ian Smith. Nimepoteza miaka yangu 15 nikipigana dhidi ya dhuluma katika nchi yangu.

“Ian Smith anahusika na vifo vya watu wasiopungua 50,000 katika nchi yangu. Nina makovu ya ufidhuli wake ambao Marekani na Uingereza zilikuwa zinautetea. Ninakutana na waathirika wa ufidhuli huo kila siku, lakini bado mtu huyo anatembea huru. Anaendesha kilimo kwa uhuru. Ana shamba la zaidi ya ekari 500. Anaongea kwa uhuru na kukutana na watu kwa uhuru chini ya Serikali ya watu weusi.

“Tumemfundisha demokrasia. Tumemrudishia utu wake. Angekutana na mikasa hapa au Ulaya kama watu 50,000 (Wazimbabwe) alioua wangekuwa Wazungu. Afrika haijataka kuita mkutano wa kujadili mauaji yaliyofanyiwa watu weusi na Wazungu .

“Haijaanza kusaka wauaji wa Kimbari ambao baadhi wanaishi hadi leo wala kudai fidia kwa mateso hayo. Badala yake ni Afrika ndiyo inatiwa hatiani leo hii. Ni Mugabe na si Waziri Mkuu wa Uingereza ndiye anatiwa hatiani akituhumiwa na dunia ile ile iliyoifanya ufidhuli Afrika kwa karne kadhaa,” Rais Mugabe alisema Rais Bush anaonekana amejisahau kabisa na kudhani yuko juu ya sheria zote.

Awali Rais Mugabe alitoa shukrani kwa Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na viongozi wa mataifa ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kufanikisha mazungumzo ya mapatano baina ya chama tawala ZANU-PF na chama kikuu cha upinzani cha MDC. Matokeo ya mazungumzo hayo ni makubaliano yaliyowezesha Bunge la Zimbabwe kupitisha marekebisho ya Katiba ya Zimbabwe Jumanne iliyopita Septemba 25, 2007.

“Hatustahili kuwekewa vikwazo, sisi ni Wazimbabwe na tunajua jinsi ya kumaliza matatizo yetu. Tumefanya hivyo huko siku za nyuma hata kabla ya Bush na Brown hawajajulikana katika siasa.
“Tuna jumuiya na mshirikisho yetu ya Bara zima na Kanda. Na kwa kupitia huko napenda kutoa shukrani za dhati kwa Rais Thabo ambaye kwa niaba ya SADC amefadhili na kufanikisha vikao kati ya chama tawala na vyama vya upinzani na kuleta matokeo tunayoona,”

Pamoja na hali aliyokumbana ya kujiuzulu na kuondoka kwa fedheha kusema kwake ukweli kuhusu vitendo vya kikandamizi kutoka kwa nchi za Magharibi kunabakia kuwa moja ya mambo muhimu aliyochangia katika kuzitaka nchi hizo ziheshimu rasilimali za Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles