Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
MTUNZA bustani Maganga Masele (25), mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais Dk. John Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan.
Kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage na imesomwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Lucy Mallya.
Akisoma mashtaka hayo, Lucy alidai kuwa Desemba 22, mwaka jana, maeneo ya Leaders Club, Kinondoni, mshtakiwa aliwatukana viongozi hao matusi ya nguoni na kudai kuwa wanaendesha nchi kinyume na maumbile.
Mshtakiwa alikana mashtaka na kupewa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja na ahadi ya Sh milioni 5.
Upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kesi hiyo itatajwa tena Januari 24, mwaka huu.
Aprili mwaka jana, mkazi wa Olasiti jijini Arusha, Isaac Emily (40), alipandishwa kizimbani kwa kutoa lugha chafu na kumdhihaki Rais Magufuli katika mitandao ya kijamii.