JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA
WAKATI wazazi wa Xiao Feng walipompeleka mtoto wao hospitali walikuwa na wasiwasi na tatizo la ugumu wa kupumua na kuvimba kwa tumbo lililomkabili.
Hawakuwa wakitarajia kuwa madaktari watakuta kitu kingine wakati walipomfanyia vipimo, ikabainika Feng alikuwa na mimba ya pacha wake.
Mvulana huyo mwenye umri wa miaka miwili mkazi wa wa Huaxi nchini China, alipelekwa hospitali baada ya tumbo lake kuwa kubwa kiasi ambacho alijikuta akishindwa kupumua.
Mvulana huyo alipolazwa, madaktari walichukua picha za x-rays na MRI na kugundua kuwa alikuwa amebeba mimba isiyokua na hivyo kuamua kumfanyia upasuaji kuiondoa.
Waliiondoa mimba hiyo changa iliyokuwa na upana wa sentimita 20 na tayari ilikuwa imeanza kuwa na vidole.
Mimba hiyo ilitakiwa kuwa pacha wa mtoto huyo (yaani mmoja alikulia tumboni mwa mwenzie). Pacha huyo wa sponji angekua na kuwa mtoto wa kiume.
Mapacha wanaofanana hutokea pale yai linapojigawa wakati wa urutubishaji ilihali mapacha walioungana hutokea pale yai linaposhindwa kujigawa.
Katika kesi ya Feng, kijusi kilichoondolewa kilikuwa pacha aliyeungana aliyejipenyeza ndani ya mwili wake.
Madaktari wanasema ilibidi wakiondoe kijusi kwa vile bila kufanya hivyo Feng angekufa siku za usoni.
Ijapokuwa kesi hii iliyotokea mwaka 2013 inaweza kuwa ya kushangaza au ajabu lakini si mpya.
Mwaka 2012 nchini Peru, mvulana mwenye umri wa miaka mitatu alikutwa akiwa amebeba mimba ya pacha wake, kwa mujibu wa Shirika la Habari la CBS la Marekani.
Aidha, mwaka 2008, kulikuwa na kesi kama hiyo ikihusisha msichana mwenye umri wa miaka tisa raia wa Ugiriki, ambaye alikuitwa na uvimbe ambao ukafahamika kuwa ni pacha.