Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amewaagiza viongozi wa serikali kuanzia mamlaka za chini kutokuwa kikwazo kwa wafanyabiashara ndogo ndogo jijini humo badala yake wawe sehemu ya kuwawezesha kukua kibiashara na kufikia malengo yao.
Mtaka ametoa kauli hiyo jana Julai 4, alipokutana na wafanyabiashara ndogo ndogo jijini humo ambapo pamoja na mambo mengine, amesikiliza kero na changamoto zinazowakabili katika biashara zao.
“Lakini pia na ninyi wafanyabiashara nawasihi kuzingatia sheria na kanuni za kufanya biashara ili msilete athari kwa wananchi wengine wakati wa kutimiza majukumu yenu,” amesema.
Katika mkutano huo pia wafanyabiashara wadogo waliiomba serikali iwapange vizuri katika maeneo hayo na kurasimisha baadhi ya maeneo ili wasipate bugudha kutoka kwa askari na migambo wa jiji.
Mkutano huo uliowakutanisha Wafanyabiashara wadogo kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma, ulihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa Dk. Fatma Mganga, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dodoma,Wakuu wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.