Na JOACHIM MABULA,
VIJANA wanapobalehe au kuvunja ungo wanapitia hatua mbalimbali za ukuaji ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya hisia. Vijana huwa wepesi kujihusisha na tabia hatarishi kama ngono na matumizi ya vilevi mbalimbali. Tabia hatarishi kama ngono isiyo salama husababisha watoto wa kike kushika mimba na kupatwa na magonjwa ya ngono ikiwa pamoja na Virusi vya Ukimwi (VVU).
Wasichana wanapokuwa wajawazito masomoni hukataliwa na waliowapa mimba, wengine wakishawishiwa kutoa mimba na ikigundulika wana mimba katika uongozi wa shule hufukuzwa na kurudi nyumbani ambapo wazazi wanakuwa wamechukizwa na hali hiyo, hivyo kuwafanya watoto kushikwa na msongo wa mawazo.
Msongo wa mawazo ni hali ya mtu kusongwa na mambo mengi kichwani kutokana na tukio au jambo fulani hasa baya lililotokea, linalotokea au lilotarajia kutokea. Mtu akiwa na msongo wa mawazo anakuwa na ugonjwa wa akili unaosababisha tabia ya mtu kubadilika na kuishi tofauti na jamii inayomzunguka.
Tatizo hili huwapata watu wa rika na jinsi zote ingawa vijana wanaobalehe au kuvunja ungo, wazee na wajane wapo katika hatari zaidi ya kupata msongo wa mawazo. Mambo kama shinikizo la marika, matarajio ya wazazi na matukio ya kuumiza huchangia msongo wa mawazo kwa vijana wa shule.
Mara nyingi mtu mwenye msongo wa mawazo hupatwa na hali ya kiakili na ubongo inayoharibu jinsi unavyofikiri na kubadili tabia, pia mgonjwa huwa na hisia hasi ambazo huathiri utendaji wa mwili wake kama alipatwa na tukio la kusikitisha. Mgonjwa huendelea kusikitika na kutokuwa na furaha hivyo watu hudhani anasikitika tu.
Nini husababisha msongo wa mawazo?
Kiujumla mtu anapopoteza mambo au vitu alivyoviona vina maslahi na thamani kubwa maishani mwake humfanya kupatwa na msongo wa mawazo. Mambo hayo ni pamoja na kupata ujauzito shuleni, kuachana na mpenzi au mwenza wa ndoa, kuachishwa kazi, kustaafu kazi huku ukiwa hujajiandaa na maisha ya bila ajira, kufiwa na mtu unayempenda, kufungwa gerezani, kupatwa na ajali mbaya na kuugua.
Mambo mengine ni kufilisiwa kutokana na mikopo, kubadili mazoea ya kulala, kuhamia sehemu nyingine mbali na wale uliwazoea, kupewa majukumu ambayo hukuyazoea kama kuhubiri au kuhutubia halaiki, kubadili mazoea ya kula, hofu baada ya kuvunja sheria au taratibu na matatizo ya kibiashara kama kupata hasara.
Nitajuaje kuwa nina msongo wa mawazo?
Kimsingi ugonjwa huu huathiri akili na ubongo wa mtu na kumfanya abadili tabia tofauti na mwanzo. Tabia hizo ni kama unyonge, kulia, kutokula vizuri kunakosababisha afya kudhoofu, kutopata usingizi ingawa upo kitandani muda mwingi, kuhuzunika kupita kiasi, kukaa kimya au kuchukua muda mrefu kujibu anachoulizwa, kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi, ugumu wa kufuatilia kitu kwa makini, mawazo ya kutaka kufa au kujiua.
Tabia zingine ni pamoja na kuwa na wasiwasi, kuongezeka kwa mapigo ya moyo, kuwa msahaulifu, kuwa na tabia ya kukasirika haraka, kuota ndoto za kutisha, kuumwa kichwa au kipanda uso, kiungulia au kuharisha, kutokwa na jasho kwapani au kwenye viganja vya mikono, kujitenga na jamii inayokuzunguka, kutopata hedhi au kupata hedhi isivyo kawaida, kupata shida katika uongeaji, vidonda vya tumbo na kuumwa mara kwa mara.
Matibabu ya msongo wa mawazo
Mgonjwa wa msongo wa mawazo anapopelekwa kituo cha kutolea huduma za afya madaktari humfanyia uchunguzi wa kimwili ambapo hawaoni maradhi anayoumwa. Baadhi ya madaktari wasio na ujuzi na magonjwa ya akili hufikiri mgonjwa amerogwa au ana mapepo.
Watu wanapokosa matibabu ya mgonjwa wao hukimbilia kwa waganga wa kienyeji kwa msaada zaidi na wasipofanikiwa huamua kufuata msaada kwa viongozi wa dini kwa ajili ya maombezi ili kuondoa mapepo yanayomsumbua muumini wao.
Ikiwa mgonjwa wa msongo wa mawazo atafika kituo cha huduma za afya na kukutana na mtaalamu wa magonjwa ya akili, matibabu yatahusisha ushauri nasaha na dawa za akili ambazo zitamponya na kurudisha hali yake ya mwanzo.
Ushauri nasaha unasaidia mgonjwa kuelewa hali yake na jinsi ya kujiondoa kwenye tatizo. Mtaalamu wa afya atampangia mgonjwa ratiba ya kuhudhuria hospitali mara nyingi zaidi mwanzoni na hupunguza idadi ya mahudhurio jinsi mgonjwa anavyoimarika.
Dawa za msongo wa mawazo hufanya kazi kwenye akili na ubongo. Ni muhimu kumvumilia mgonjwa, usimtegemee kuanza kuwa kama zamani muda wowote hivi punde. Mgonjwa anahitaji muda wa kutosha kurudi katika hali yake ya kawaida.
Athari zake
Msongo wa mawazo huathiri maisha ya kila siku ya mtu kwa maana tabia hubadilika. Huweza kusababisha kushuka kwa kinga ya mwili na ni matokeo ya kuongezeka kwa kichocheo cha cortisol. Athari zingine ni kupungua kwa ufanisi katika utendaji kazi, kupatwa vidonda vya tumbo kwa sababu ya kutokula, kuvunjika kwa ndoa na familia, kuongezeka kwa vitendo vya kigaidi na kujitoa muhanga na ajali.
Ufanye nini ili kuepuka msongo wa mawazo?
Ili kuzuia tatizo hili, mtu anahitaji kuwa na maisha yenye ratiba, malengo na kushirikiana na watu vizuri. Wataalamu wa magonjwa ya akili wanashauri uwe mwenye utaratibu, panga ratiba unayoweza kutimiza, kukubaliana na hali halisi endapo hauna uwezo wa kubadilisha mambo kama jinsi ulivyoumbwa iwe mrefu au mfupi, kifo, ajali na ulemavu wa kudumu.
Ushauri mwingine kula vyakula vinavyofaa kwa ukawaida, fanya mazoezi yanayofaa, weka miradi unayoweza kufikia na usitarajie ukamilifu, pumzika vya kutosha (pata usingizi wa kutosha), kuwa na fikra chanya, kuwa na uhusiano mzuri na watu wanaokuzunguka kwa kujiunga na vikundi au vyama vya kijamii ambako utapata marafiki na ukisumbuliwa na jambo fulani mweleze mtu unayemwamini.