Na Mwandishi Wetu, Geita
Mageuzi makubwa katika sekta ya madini yameifanya sekta hiyo kuendelea kuongeza mapato ya Serikali kutoka Sh bilioni 194.6 ilizokusudia kukusanya mwaka 2017/2018 hadi kufikia Sh bilioni 301.6 ikiwa ni ongezeko la asilimia 55.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Serikali.
Alisema ongezeko hilo la mapato katika madini limechagizwa na mabadiliko katika sheria za madini, kujengwa kwa ukuta wa Mirerani na kuzuia kwa usafirishaji wa mabaki (kaboni) ya dhahabu nje ya mkoa yanapochimbwa madini.
“Rais John Magufuli aliagiza kujengwa ukuta eneo la wachimbaji wadogo la Mirerani na Aprili, mwaka huu ukuta huo ulikamilika na kuwezesha kuongezeka kutoka kilo 164.6 za madini ya Tanzanite yenye thamani shilingi milioni 71.8 mwaka 2016 hadi kufikia kilo 449.6 zenye thamani ya shilingi milioni 893.8 kwa kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka huu,” alisema.
Kutokana na usimamizi mzuri, alisema kampuni za uchimbaji madini yameendelea kutoa mchango wake kwa jamii na Geita Gold Mine imeipa Geita Sh bilioni 9.2 kama mchango wa kampuni hiyo kwa maendeleo ya mkoa huo.
Pia alisema zuio la kaboni zenye dhahabu kusafirishwa na kuchakatwa nje ya mkoa zinakozalishwa limesaidia kuongeza pato kwa Serikali kufikia Sh milioni 850 kwa Agosti, mwaka huu kutoka Sh milioni 400 kwa Aprili.
Mbali na hayo, alisema Wizara ya Madini imeendelea kufanya mageuzi mbalimbali ikiwamo kujenga vituo saba vya umahiri vitakavyokamilika Desemba, mwaka huu na kuwapatia wachimbaji wadogo mafunzo na utaalamu zaidi wa uchimbaji.
Kuhusu sekta ya afya, alisema uwekezaji mkubwa wa vifaa, wataalamu na majengo umefanyika katika hospitali za Muhimbili, Mloganzila, MOI, Bugando, Benjamin Mkapa na hivi sasa Tanzania inapokea wagonjwa kutoka Komoro, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia kwa ajili ya kupata matibabu ya kibingwa ya moyo, figo, mifupa na kuongeza uwezo wa kusikia.
“Serikali imeendelea kusogeza huduma za afya karibu kwa wananchi kwa kujenga hospitali za rufaa katika mikoa saba, hospitali za wilaya 67 zinajengwa mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 105 na tayari vituo vya afya 210 pamoja na nyumba za wahudumu wa afya vimejengwa,” alisema.