NAIROBI, KENYA
SIKU moja tu baada ya mwili wa Kaimu Mkurugenzi wa Teknohama wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Chris Msando kupatikana akiwa amefariki dunia baada ya awali kutoweka, Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Kanali Joseph Owuoth, amejitokeza na kuzishangaa ripoti zinazodai naye ametoweka.
Kanali Owuoth amesema yeye ni mzima wa afya na anaendelea na majukumu yake.
Alisema kuwa hayuko Kisumu kama inavyodaiwa na kwamba taarifa hizo za uzushi zipuuzwe.
“Ni mzima na sielewi zinakotoka ripoti hizi,” alisema.
Kauli yake imekuja saa chache baada ya familia yake kudai kuwa imeshindwa kumpata.
Familia pia ilidai Kanali Owuoth alipewa likizo ya lazima kupisha uchunguzi kuhusu nyaraka za siri za jeshi zilizochapishwa na upinzani wiki iliyopita.
Taarifa hizo zinakuja siku moja tu baada ya kundi la wanasiasa wa upinzani, National Super Alliance (Nasa) kuitisha mkutano wa wanahabari kudai kuwa Kanali Owuoth amesimamishwa.
“Amepewa likizo ya lazima na kuamriwa kurudi nyumbani kwake Kijiji cha Koru,” alidai Seneta wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o katika mkutano na wanahabari mjini humo.
Nyong’o, ambaye kwa sasa anawania ugavana wa Kisumu, alidai kuwa Kanali Owuoth alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na dada yake Elizabeth hadi jana (juzi) wakati alipokuwa Nakuru, lakini sasa familia haimpati.
Hata hivyo, pamaja na ripoti hizo, simu yake ilikuwa hewani sawa na akaunti yake ya WhatsApp ijapokuwa ujumbe aliokuwa akitumiwa haukuwa ukijibiwa.
Kanali Owuoth alijiingiza katikati ya utata baada ya vinara wa Nasa kuanika nyaraka zinazolituhumu jeshi kupanga njama za kukisaidia Chama cha Jubilee kubaki madarakani kwa lazima.
Operesheni hiyo, kwa mujibu wa nyaraka ni pamoja na kukata umeme na usambazaji wa maji katika baadhi ya maeneo, kuandikisha askari wapya wa kudhibiti umati, kuweka makamanda rafiki wa Jubilee na mengineyo ambayo upinzani ulisema utawafanya wafuasi wake kutojitokeza kupiga kura.
Kanali Owuoth badaye alithibitisha uhalisia wa nyaraka hizo, lakini aliwatuhumu wanasiasa kwa kupotosha maudhui ya operersheni hiyo kwa malengo ya kisiasa.
Lakini baadaye Waziri wa Ulinzi, Raychelle Omamo, alizikana nyaraka hizo, akisema hajaziona na kuwa KDF haina njama zozote zilizo nje ya sheria.