LAGOS, NIGERIA
Kiongozi wa ofisi ya rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari aliyetajwa kwa jina la Abba Kyari amefariki baada ya kupatikana na virusi vya Corona.
Kupitia taarifa iliyotolea na ofisi ya Buhari imesema imesikitishwa na kifo cha Abba Kyari ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa katika utawala wa Rais huyo.
Taarifa hiyo imesema kuwa marehemu alifariki juzi Ijumaa kutokana na ugonjwa wa COVID-19.
Kyari aliyekuwa katika miaka ya sabini, ni mtu wa kwanza mwenye cheo cha juu nchini Nigeria kufariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19.
Nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, imethibitisha visa 493 vya maambukizi ya virusi vya Corona na vifo 17.
Haijabainika wazi iwapo Rais Buhari amefanyiwa vipimo vya iwapo ameambukizwa virusi vya Corona, lakini mara kwa mara amekuwa akitoa hotuba akisisitiza kuwekwa vizuizi ili kupunguza kuenea kwa virusi hivyo.
Shirika la Fedha Duniani IMF limetoa wito wa msaada wa haraka wa kimataifa kwa nchi za Afrika baada ya juzi WHO kutoa onyo kuwa Afrika inaweza kuwa kitovu na maambukizi mapya ya corona katika kipindi kifupi kijacho baada ya kuripoti kesi nyingi mpya ndani ya wiki moja.
IMF, pamoja na viongozi wa Afrika na Benki ya Dunia wametoa wito huo wakati ambapo janga hilo linatarajiwa kusababisha uchumi wa bara hilo kushuka kwa asilimia 1.25 mwaka huu wa 2020.
Mkurugenzi mkuu wa IMF, Kristalina Georgieva amewaambia mawaziri, maofisa wa Umoja wa Mataifa na wengine kwamba bara la Afrika halina raslimali za kutosha na miundo mbinu ya kutosha ya afya ili kukabiliana na janga hilo na kwamba linahitaji karibu dola bilioni 114.
Katika mkutano wa msimu wa machipuko wa Benki ya Dunia na IMF uliofanyika kwa njia ya video, maofisa wameelezwa kuwa licha ya ahadi zilizotolewa bado kuna mapungufu za dola bilioni 44.
Umoja wa Mataifa unasema ugonjwa wa virusi vya corona unatarajiwa kusababisha vifo laki tatu katika bara la Afrika.
WHO limesema huenda nchi nyingi za Afrika zikaufuata mkondo wa China na kuangazia upya idadi ya vifo.