29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

MPUKUTIKO ACT-WAZALENDO

Na AGATHA CHARLES

KUONDOKA kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi na kabla ya hapo Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Samson Mwigamba, kunaiacha wazi safu ya juu ya uongozi wa chama hicho iliyokuwa ikiundwa na waanzilishi wake wengi wakiwa ni wale waliotoka Chadema.

Hatua ya Mwigamba na wenzake tisa kuondoka na kutangaza kurejea Chama Cha Mapinduzi  (CCM), kwa madai mbalimbali, ikiwamo baadhi ya viongozi wa ACT- Wazalendo wamekuwa wakikiuka misingi ya kuanzishwa kwake, ni  mwendelezo wa viongozi wa juu wa chama hicho kuondoka kwa sababu mbalimbali.

Katika kipindi cha takribani miezi sita, ACT-Wazalendo si tu kimepoteza viongozi wake wanne, bali waasisi wa chama hicho, ambapo wawili waliteuliwa kushika nyadhifa tofauti serikalini.

Viongozi hao, ambao wote walitoka Chadema, ni aliyekuwa Mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo, ambaye Aprili, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alimteua kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Uteuzi huo haukuishia hapo, kwani Juni mwaka huu, Rais Dk. Magufuli alimteua aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Mshauri wa Sheria, Albert Msando, naye alitangaza kujiuzulu, kutokana na kashfa za picha mtandaoni.

Kutokana na hilo, safu ya uongozi wa juu iliyokuwa inaongozwa na waanzilishi wake ni kama amebaki Zitto Kabwe peke yake, ambaye ndiye Kiongozi wa chama.

Mwigamba, ambaye kwa sasa ndiye anayeonekana kuzidisha ufa zaidi katika safu ya uongozi ndani ya ACT, alikuwa Katibu Mkuu, kabla ya mwaka jana kujiuzulu na kwenda masomoni, na aliporejea alikaimu kwa muda nafasi ya Mghwira na baadaye kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdalah Khamis, alifafanua hilo kuwa kati ya walioondoka ni nafasi moja tu ya kupigiwa kura (Mghwira), huku nyingine zikiwa za kuteuliwa.

“Tungekuwa tunakwenda kwenye uchaguzi, tungelazimika kuziba kwa kuchagua Mwenyekiti, lakini tayari kuna mtu kateuliwa kuziba na inakaimiwa kwa mwaka mmoja,” alisema Khamis.

Aliwataja wanaoshikilia nafasi hizo kwa sasa kuwa ni Kaimu Mwenyekiti Taifa, Yeremia Maganja, Makamu Mwenyekiti Bara, Shaaban Mambo, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Juma Sanani.

Katika nafasi nyingine ni Kaimu Katibu Mkuu Doroth Semu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Msafiri Mtemelwa na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Hamad Mussa Yusuf.

Akizungumzia kiini cha kuondoka kwa Mwigamba, Khamis alisema ni muda mrefu alikuwa akipingana na hatua ya ukosoaji iliyokuwa ikifanywa na Zitto kuhusu serikali ya awamu ya tano.

Alisema hata Zitto alipokosoa hatua ya madiwani watano kukihama Chadema na kuhamia CCM, Mwigamba aliipinga hoja hiyo.

Itakumbukwa kuwa Zitto, Profesa Kitila na Mwigamba, ndio walikuwa waasisi wa ACT-Wazalendo, baada ya kufukuzwa Chadema kwa usaliti katika kipindi cha mwaka 2014-2015.

Vuguvugu hilo lilianza Novemba mwaka 2013, baada ya Zitto kuvuliwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, huku Profesa Kitila akivuliwa nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu.

Uamuzi huo wa Kamati Kuu ulitangazwa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye alisema wawili hao pamoja na Mwigamba, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, walikuwa na mtandao wa kukiua Chadema na kutengeneza tuhuma za kuwachafua Mwenyekiti Freeman Mbowe na aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa.

Katika makosa waliyokutwa nayo ni kubainika kwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, ulioandaliwa na kikundi hicho kilichomjumuisha Zitto, akiwa ndiye MM, Profesa Mkumbo (M1) na Mwigamba M3, huku M2 akishindwa kupatikana hadi leo na huenda amebaki Chadema.

Baadaye Januari 2014, Dk. Slaa alitangaza maamuzi ya Kamati Kuu na kuwavua uanachama Mwigamba na Profesa Kitila, huku Zitto akiwa na kinga ya mahakama.

Hata hivyo, Machi 2015, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitupilia mbali kesi iliyofunguliwa na Zitto dhidi ya Chadema kuhoji uhalali wa uanachama wake na hivyo Lissu alitangaza rasmi kuvuliwa kwake uanachama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles