Na BADI MCHOMOLO
UKIZUNGUMZIA kundi la muziki wa Regge la Morgan Heritage kwa muziki wa Bongo Fleva ni jina geni kidogo, lakini linaanza kuenea kwenye midomo ya watu.
Lilikuwa linajulikana kwa muda mrefu tangu mwaka 1994 lilipoanzishwa, lakini wengi walikuwa hawalifuatilii sana hasa kutokana na aina ya muziki wanaofanya.
Nyota wa muziki hapa nchini Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ ameweza kuwakumbusha mashabiki wa kundi hilo, huku wengine wakianza kulijua kundi hilo kupitia msanii huyo baada ya kufanya nao kazi kwenye wimbo wake wa Hallelujah.
Ni wimbo ambao unafanya vizuri kwa sasa hasa kutokana na wasanii wa kundi hilo kutenda haki katika vipande walivyoshiriki.
Morgan ni jina la familia kutoka kwa mzee Denroy Morgan, hivyo mzee huyo aliwashauri watoto wake kutumia jina hilo ili kuweza kulifanya lidumu kwa miaka mingi.
Hata hivyo aliwaambia wanatakiwa kulirithi jina hilo, hivyo wakaamua kujiita Morgan Heritage, wakiwa na maana Urithi wa Morgan.
Morgan Heritage ni kundi la wasanii watano kutoka familia moja ya muziki, baba yao Morgan alikuwa nyota wa muziki huo wa Reggae miaka ya nyuma.
Kundi hilo linaundwa na Peter ‘Peetah’ Una, Gramps, Nakhamyah ‘Lukes’ na Memmalatel ‘Mr. Mojo’ wote ni watoto wa mzee Morgan.
Walifanya mapinduzi makubwa kwenye muziki huo mwaka 1998 baada ya kuanza kuonekana kwenye shoo yao ya kwanza ya Reggae Sunsplash ambayo ilifanyika nchini Jamaica.
Walizaliwa nchini Marekani, lakini muziki ambao wanaufanya ulikuwa unakubalika kwa kiasi kikubwa nchini Jamaica. Hata hivyo familia yao ilitokea nchini humo miaka ya nyuma.
Kutokana na kukubalika sana nchini Jamaica, kundi hilo liliona bora kwenda nchini Jamaica kwa ajili ya kufanya biashara ya muziki huo, lakini wasanii watatu kwenye kundi hilo wakaamua kugoma kwenda Jamaica na kuamua kujitoa kwenye kundi huku wakidai kwamba wanataka kubaki nchini Marekani.
Hata hivyo kujitoa kwao hawakumaanisha kuwa wanavunja kundi, walikubaliana kuwa watafanya kazi pamoja lakini hawakukubaliana kuishi Jamaica.
Wawili waliokwenda nchini Jamaica walifanikiwa kufanya kazi na prodyuza mwenye uwezo wa juu nchini humo ambaye akijulikana kwa jina la Bobby Dixon na Lloyd James na kufanikiwa kuachia albamu yao ikijulikana kwa jina la ‘Protect Us Jah’ wakimaanisha ‘Mungu tulinde’ ilitoka mwaka 1997.
Albamu hiyo ilizidi kuwapa jina kubwa, hivyo walianza kufanya ziara ya muziki bara la Ulaya na kuamua kuungana na wale watatu ambao waligoma kuishi Jamaica.
Baada ya kuungana waliweza kutengeneza albamu zingine nyingi kama vile One Calling (1998), Don’t Haffi Dread (1999).
Wakiwa katika ziara yao ya muziki barani Ulaya, mwaka 2003 waliachia nyimbo mbili, moja iliitwa ‘Live In London’ na ‘Live Over Europe’
Kutokana na nyimbo hizo mbili kufanya vizuri, walipata nafasi ya kufanya kazi na wasanii wenye majina makubwa duniani kwenye muziki wa Reggae kama vile Capleton, Junior Kelly, Luciano, Gentleman na Beres Hammond.
Kutokana na kufanya kazi na baadhi ya wasanii hao, walibahatika kupata nafasi ya kuwania tuzo za Grammy mwaka 2015 nchini Marekani.
Walifanikiwa kutwaa Tuzo ya Albamu Bora ya Mwaka kupitia albamu ya Strictly Roots walioiachia mwaka 2015.
Tangu wafanikiwe kuchukua tuzo hiyo hadi sasa wanaendelea kufanya vizuri kutokana na albamu yao mpya ya Avrakedabra iliyoachiwa Mei 19 mwaka huu.