NA SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM
MWEKEZAJI wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji maarufu Mo, amesema anafahamu kuna watu wana lengo la kumkatisha tamaa ili ajiondoe katika klabu hiyo, lakini amesisitiza kuwa kamwe hatachukua uamuzi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mo ambaye pia ni mwanachama klabu hiyo alisema pamoja na misukosuka anayokutana nayo kwenye uwekezaji wa klabu hiyo, ataendelea na mipango yake ya kuhakikisha inakuwa bora barani Afrika.
“Arsenal inapofanya vibaya siumii kama ikifanya vibaya Simba kwasababu naipenda.
“Wapo wanaohoji bilioni 20, uwezi kuingiza fedha wakati kuna mambo hayajakamilika, kuna suala la kuhamisha madeni kutoka Simba SC kwenda Simba Sports Club Limited.
“Pamoja na kutokamilika kwa baadhi ya vitu, mimi ndio nitayetoa hela kuanzia usajili , awali bajeti ya Simba ilikuwa milioni mia sita lakini sasa imeongezeka kwa asilimia mia moja.
“Nahahamu asilimia tisini ya Wanasimba wanakubali jitihada zangu za kuhakikisha inakuwa klabu kubwa barani Afrika,”alisema Mo.
Alisema amekuwa akiisaidia Simba kwa muda mrefu na kwa mapenzi yake binafsi bila kujali nini anapata kutoka kwa klabu hiyo, tofauti na baadhi ya watu aliowaita wasaliti wanavyomchukulia.
“Hata waseme nini, mimi siwezi kuondoka Simba, nitaendelea kuisaidia ili kuendelea kuwapa raha Wanasimba. Hata mimi mwenyewe, Simba inapofanya vibaya, huwa naumia sana, hivyo siwezi kuiacha Simba yangu kirahisi hata, wanaonisakama wanajisumbua bure, siondoki Simba ng’o,” alisisitiza Mo Dewji.
Mfanyabiashara huyo alisema kuwa Wanasimba wanatakiwa kujivunia kwa maendeleo yaliyofikiwa na klabu yao kwa sasa, ikihesabika kama moja ya klabu kubwa Afrika.
“Wenyewe mmesikia Barbara (Gonzalez) alivyopongezwa na FIFA na CAF baada ya kuchaguliwa kuwa C.E.O (Ofisa Mtendaji Mkuu) mpya wa Simba, hili si jambo dogo, ni kutokana kazi kubwa ambayo tumeifanya ya kuijenga Simba, hilo wapenzi wenzangu wa Simba lazima walifahamu,” alisema.
Wakati huo huo Mo aliwataka mashabiki wa timu pinzani ya Yanga kuwasapoti watakaposhiriki michuano ya kimataifa kwa maslahi mapana ya Tanzania.
“Sisi Simba tukifanya vizuri Tanzania inaweza kupanda hadi nafasi ya 12 ambayo itakuwa ni faida hadi kwa Yanga.
“Hili wanatakiwa waliangalie wenzetu badala ya kutuombea tufanye vibaya wakati wao hawawezi kutwaa ubingwa wa ligi na kupata fursa ya kushiriki michuano ya kimataifa.
“Haipendezi kama kila siku tutakuwa tunaenda kushiriki sisi tu,”alisema Mo.
Simba itaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tiketi iliyoipata baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba, Haji Manara, aliwataka Wanasimba kujivunia maendeleo yaliyofikiwa na klabu yao kwa sasa chini ya uwekezaji wa Mo Dewji.
“Wanasimba wenzangu tusiyumbishwe, tukumbuke tunakotoka, Simba tulikuwa na hali mbaya sana miaka ya nyuma, kuna wakati hata fedha za nauli ya kuisafirisha timu ilikuwa ni shida.
“Nakumbuka kuna wakati nilikuwa nikisafiri na timu mikoa kama Kagera, inabidi tusimame Dodoma tuwaombe wabunge watuchangie, tena hadi wabunge wa Yanga walikuwa wanatuchangia. Watachanga laki laki, tunapata pesa ya kutufikisha na posho kidogo kwa wachezaji,” alisema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Tyr Again’, aliwataka Wanasimba kutokubali kuyumbishwa na watu wenye nia ya kuwarudisha nyuma kimaendeleo wakati tayari wameanza kupiga hatua kubwa.