Faraja Masinde -Dar Es Salaam
KATIKA kuhakikisha kuwa ugonjwa wa saratani unaendelea kudhibitiwa nchini Taasisi ya Mo Dewji Foundation imetoa msaada wa Sh milioni 100 kwa Tumaini La Maisha (TLM) asasi isiyo ya kiraia inayofanya kazi na Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa huduma na matibabu kwa watoto wenye saratani nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo jana Dar es Salaam, msaada huo ni sehemu ya kujitolea kwake kila mwaka katika kuboresha ustawi wa huduma na matibabu kwa
watoto wenye saratani nchini.
Kituo cha kitaifa cha saratani cha watoto kilichopo Muhimbili ni wodi ya kwanza ya watoto wenye
saratani nchini.
“TLM ilianza na jukumu kabambe kuhakikisha wagonjwa katika wodi ya watoto wanapokea huduma bora na za hali ya juu ambapo matibabu yanatolewa bure pamoja na gharama za usafiri kutokea mahali popote nchini.
“Tangu, Mohammed Dewji alipotembelea kituo hicho kwa mara ya kwanza 2015, ameahidi mchango wa kila mwaka kuboresha juhudi ya kugharamia vifaa tiba na dawa, pamoja na vifaa vipya, lakini pia kusaidia programu za kliniki,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TLM ilizinduliwa na kusajiliwa Novemba 2011 nchini lengo likiwa ni kwa watoto
wote wenye saratani nchini kupata huduma bora zinazosaidia uponyaji unaofanana na nchi zilizoendelea, na kuhakikisha hakuna mtoto nchini Tanzania anayeteseka au kufariki kwa
saratani.
“Timu yetu imekua kutoka chumba kimoja Taasisi ya Saratani ya Ocean Raod(ORCI) hadi kuwepo hospitali ya taifa(MNH) pamoja na vituo nane vya ushirika kote nchini.
“Mo Dewji Foundation itaendeleza msaada wake wa Tumaini La Maisha na kuhimiza wengine kufanya hivyo, tunaamini kuimarisha mifumo ya afya itasaidia kuboresha maisha ya Watanzania. Tunawahimiza Watanzania wote kuunga mkono juhudi muhimu za TLM na asasi zingine zisizo za kiserikali zinazofanya kazi kuwawezesha wananchi wengi wanaoishi katika mazingira
magumu nchini,” ilieleza taarifa hiyo.
Itakumbukwa Februari, mwaka huu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizindua rasmi muongozo wa taifa wa tiba ya saratani mbali na kuihasa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kuendeleza na kutoa elimu za visababishi, dalili za kutambua saratani na kile kinachopaswa kufanyika pale ambapo tayari mtu anapokuwa amegundulika na ugonjwa wa Saratani pia alieleza takwimu za ugonjwa huo kwa hapa nchini na duniani kwa ujumla.
“Kwanza kabisa napongeza juhudi kubwa zilizopo nchini za kuongeza hospitali za kutibu wananchi dhidi ya ugonjwa wa Saratani, kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika kila watu 100,000 kuna wagonjwa 76 wapya wa saratani.
Huku vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo kufikia 68 kwa kila wagonjwa 100. Hali hii ya vifo inatokana hasa na wagonjwa wengi kuhudhuria hospitali wakiwa katika hatua ya mwisho,” alisemaWaziri Ummy.