26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mnyukano kesi ya Wenje, Kafulila

Untitled-2Judith Nyange, Mwanza na Editha Karlo, Kigoma

KESI namba 3 ya mwaka 2015 ya kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Nyamagana, imeanza kusikilizwa huku kiapo cha ushahidi wa aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ezekiel Wenje, kikiwekewa pingamizi.

Katika kesi hiyo, Wenje anapinga matokeo yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo hilo, Stansaus Mabula (CCM), ambapo washtakiwa wengine wakiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Nyamagana.

Wakati hayo yakiendelea kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa  Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), imeshindwa kuanza kusikiliza ushahidi wa mlalamikaji, kutokana na mashahidi kutokula viapo.

Pamoja na hali hiyo taarifa kutoka jijini Mwanza zinaeleza kwamba kesi hiyo imekuwa ikivuta hisia na kuhudhuriwa na wafusi wengi wa Chadema ambao wamekuwa wakifurika mahakamani hapo kwa maandamano.

Kutokana na hali hiyo ulinzi mkali wa Polisi waliokuwa na silaha hasa wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wamekuwa na kibarua kizito cha kufanya doria mahakamani hapo.

Wenje ambaye alikuwa anapaswa kutoa ushahidi, alijikuta akigonga ukuta baada ya kuwekewa pingamizi katika aya sita zilizopo katika kiapo cha ushahidi wake baada ya  mawakili wa Mabula, Serikali na msimamizi wa uchaguzi kudai zinajenga hoja mpya katika kesi hiyo ambazo hazijatamkwa katika kesi ya msingi.

Baada ya mawakili wa Mabula, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Nyamagana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia kiapo hicho walidai kubaini kuwepo kwa upungufu mkubwa wa kisheria katika kiapo hicho.

Mawakili hao waliwasilisha ombi hilo mbele ya mahakama kuomba kuahirishwa kwa muda wa saa mbili  ili waweze kuisaidia mahakama kuhusu mambo yanayotakiwa kuondolewa katika kiapo hicho kabla hakijaanza kutumika kwa mujibu wa sheria.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Sumbawanga, Kakusulo Sambo, anayesikiliza shauri hilo alikubaliana na maombi ya mawakili hao na kutoa muda wa saa mbili kwa mawakili hao ili waweze kuisaidia mahakama kuhusu mambo ya kisheria yaliyopo katika kiapo hicho.

Wakati wakitoka mahakamani hapo Wenje akiwa ameandamana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, walisindikizwa na wafuasi wao huku shughuli zikisimama kwa muda hali iliyowalazimu askari polisi kuwadhibiti wafusi hao wasilete vurugu.

Baada ya muda huo kupita  Wakili Mkuu wa Serikali, Vicent Tango, anayemwakilisha Msimamizi wa Uchaguzi  na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alisema mahakama inatakiwa ipokee ushahidi wa kiapo katika mashauri ya uchaguzi badala ya ushahidi wa mdomo  ili kurahisisha usikilizwaji wa kesi.

Alisema viapo  hivyo ni vyema  viendane na kanuni  na sheria za viapo, hivyo kiapo kilichowasilishwa  kimejikita katika hoja  za maoni, maombi, majumuisho katika aya ya 30, 35 na 39 zinakinzana na kanuni za kisheria na hakipo sahihi kisheria hivyo waliiomba mahakama isikitumie kama ushahidi.

“Kiapo kinatakiwa kijikite kwenye mambo yanayohitaji ushahidi, hakitakiwi kuwa na maombi, hoja, maoni au majumuisho kama ilivyo katika aya 39 ambapo Wenje ameomba kurejeshewa gharama za kuendesha shauri,” alisema wakili Tango.

Kwa upande wake wakili wa mjibu maombi wa kwanza (Mabula), Costantine Mtalemwa, alisema katika kiapo hicho cha shahidi namba  tatu (Wenje) katika aya ya 31,32 na 33 kina mambo yaliyowekwa hayapo katika kesi ya msingi.

“Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi sura 243 kanuni ya 23 inaeleza kuwa  mleta maombi hatakiwi kuleta mambo yatakayosikika kwa njia ya kiapo ambayo hayapo katika madai ya msingi, naomba mahakama iondoe aya ya 31,32 na 33 ya kiapo zina ushahidi mpya ambao haupo katika madai ya msingi.

“Naomba mahakama hii isipokee ushahidi wa aya hizi kwa kuwa unatengeneza maudhui ya madai mapya ambayo hayapo katika shauri lililopo mbele yetu, naiomba mahakama iziondoe hoja hizo,” alisema Mtalemwa.

Kwa upande wake wakili wa mleta maombi (Wenje), Deya Outa, akijibu hoja hizo alisema anakubaliana na msimamo wa sheria lakini si sahihi Wakili Tango kuitaka mahakama kukikataa kiapo chote.

Alisema aya ya 31, 32 na 33 zinatoa ushahidi wa mambo yaliyopo katika aya ya 22 madai waliyoyawasilisha mahakamani kuhusu mambo yaliyoendelea katika chumba cha majumwisho.

Naye Jaji Sambo baada ya kusikiliza hoja za pande zote alisema mahakama itachunguza hoja hizo kisha  kutoa uamuzi wake kesho.

Mashahidi wa Kafulila wakwama

Kesi ya uchaguzi namba mbili ya mwaka 2015 ya kupinga matokeo ya uchaguzi katika Jimbo la Kigoma Kusini iliyofunguliwa na David Kafulila, imeshindwa kuanza kusikiliza ushahidi wa mlalamikaji, kutokana na mashahidi kutokula viapo.

Akitangaza uamuzi wa kuhairisha kesi hiyo hadi Machi 29, mwaka huu itakaposikilizwa tena Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Fedrind Wambari alisema kutokana na maombi ya wakili wa upande wa mlalamikaji kuomba muda wa kuwasilisha viapo vya mashahidi wao kabla ya Machi 18, mwaka huu kesi hiyo imehairishwa ili kupisha ukamilishaji wa jambo hilo.

Alisema baada ya mawakili wa upande wa mlalamikaji kuomba muda wa kuwasilisha viapo vya mashahidi wao kabla ya Machi 18, mwaka huu, mawakili upande wa mjibu maombi umekubaliana na ombi hilo hivyo mahakama iliridhia.

Hata hivyo, Jaji Wambari aliwasisitiza mawakili hao kuleta hati za mashahidi za kiapo zikiwa zimefungwa kwa lakiri ndipo zisomwe mahakamani.

Kesi hiyo inawavuta wananchi wengi kuja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Kigoma kuisikiliza  kwasababu ya mvuto wake kisiasa.

Awali kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa Machi 9, mwaka kwa mfululizo, lakini ilishindikana kuahirishwa mara mbili kwa sababu ya mlalamikiwa kushindwa kufika mahakamani.

Katika kesi hiyo Kafulila anawakilishwa na wakili msomi Profesa Abdala Safari pamoja na Tundu Lissu wakisaidiwa na wakili mwenyeji wa Kigoma Daniel Lumenyera.

Mbunge wa Kigoma Kusini, Hasna Mwilima (CCM), yeye anawakilishwa na wakili Kennedy Fungamtama pamoja na mawakili wa Serikali wanaomwakilisha msimamizi wa uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama washtakiwa katika kesi hiyo.

Katika  kesi hiyo,  mlalamikaji David Kafulila anaomba mahakama  imtangaze mshindi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi kifungu No112 (c) kwa hoja kwamba yeye ndiye aliyepata kura nyingi kwa mujibu wa matokeo ya kila kituo katika fomu namba 21B  na kwamba msimamizi wa uchaguzi alimtangaza Hasna Mwilima kinyume cha matokeo halisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles