NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Kibamba, John Mnyika amemuomba Rais Dk.John Magufuli kuingilia kati mradi wa maji wa Ruvu Chini maarufu ‘Bomba la Mchina’ pamoja na wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART) kuwa ni majipu sugu yanayotafuna fedha za walipa kodi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mnyika alisema siku 32 za Rais Magufuli kukaa Ikulu ametumbua vipele na si majipu kama inavyoelezwa.
Alisema tatizo la maji nchini ni kubwa ambako awali kulikuwa na nyumba inazuia mradi wa maji imebomolewa kwa sasa lakini hicho kilikuwa ni kipele na si jipu.
Katika mkutano huo, Mnyika alisema mradi huo wa mabomba ya Mchina na mradi huo wa mabasi ni majipu ambayo yanahitaji kutumbuliwa na Dk. Magufuli.
Mbunge huyo ambaye zaidi ya miaka mitano amekuwa akizungumzia tatizo la maji Dar es Salaam, alisema zaidi ya Sh bilioni 260 zimepotea katika mradi huo lakini hadi leo mabomba hayo ya Mchina hayatoi maji.
“Ni vema wahusika wachukuliwe hatua kwa vile wamesababisha maeneo yanayopata maji Ruvu Juu kama Kibamba, Msigani, Kwembe, Kimara , Tabata na kwingine kuendelea kuteseka na shida ya maji hadi leo hii,”alisema Mnyika.
Mbunge huyo alisema usambazaji wa maji ya Ruvu Juu ni ufisadi kwa kuwa kila kukicha wahusika wanasema pampu za maji zinaharibika na ripoti ya uchunguzi hadi leo imefichwa.
Usambazaji wa mabomba makubwa kutoka Mlandizi hadi Kimara ambao uligharimu Sh bilioni 89.8 hadi leo haujakamilika.
“Haya ni majipu matatu, maji ya Mchina, ripoti ya siri ya ukataji maji, ulazaji mabomba ya chini ni vema yakatumbuliwa mapema vinginevyo tutayapeleka bungeni kujadiliwa upya,”alisema Mnyika.
Kuhusu DART, Mnyika alisema mradi huo ulikuwa chini ya Ofisi ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Alisema mradi huo ambao umejaa udanganyifu ukiwamo kujengwa kwa ofisi zaidi ya 20 na kwamba mapato yatakusanywa kwa mfumo wa eletroniki, kauli hizo hazionekani kuzaa matunda.