Maregesi Paul, Dodoma
Mbunge wa Kibamba (Chadema) John Mnyika amehoji ni kwanini Wabunge hawajagawiwa ripoti ya uchunguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama kanuni za Bunge zinavyosema.
Mnyika ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma leo Aprili 12, alipokuwa akiomba mwongozo wa Spika Utawala Bora ambapo amesema kwamba kitendo cha wabunge kutogawiwa ripoti hiyo hakiwezi kuungwa mkono na wabunge kwa kuwa kinakiuka kanuni za Bunge.
Hata hivyo, ombi hilo la Mnyika liligonga mwamba baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kusema ripoti hizo za CAG haziwezi kugawiwa kwa wabunge kama Mnyika anavyotaka kwa kuwa kanuni haziruhusu kufanya hivyo.
Katika hatua nyingine Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa ameomba mwongozo na kutaka kujua ni kwanini kila Rais Dk. John Magufuli anapofanya ziara mikoani bendera za vyama vya upinzani zinaondolewa kwa nguvu na kupandishwa bendera za CCM.