Na Zuena Msuya, Arusha
WIZARA ya Madini kwa mara ya kwanza itafanya mnada wa madini ya Tanzanite ya kampuni nne za uchimbaji katika eneo la Mirerani Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Oktoba 15.
Kaimu Kamishina Msaidizi sehemu ya Uchumi na Biashara ya Madini, Godleader Shoo, alisema utaratibu wa kufanya mnada wa Tanzanite ni jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo kwenda nje ya nchi kupitia njia zisizo rasmi.
Alisema mnada huo pia utawasaidia wachimbaji kuuza madini yao kwa bei ya ushindani inayoendana na soko la dunia.
Shoo alifafanua kuwa mnada huo utashirikisha wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi, ambapo atakayefanikiwa kununua madini hayo katika mnada huo ni yule tu atakayeshinda bei iliyowekwa kwa ajili ya kununua Madini husika.
Alitaja kampuni zitakazouza madini katika mnada huo kuwa ni Kampuni ya Tanzanite One, Franone, Glitter Germs pamoja na Classic Gems ambazo zitauza madini ghafi na yale yaliyokatwa.
Akizungumzia mnada huo, Shoo alisema zoezi hilo linafanyika kwa njia ya uwazi kwa kushirikisha wachimbaji, wanunuzi, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro pamoja na Wizara ya Madini, ili kuhakikisha kuwa wauzaji na wanunuzi wa madini hayo wanapata kile wanachostahili.
“Mnada huu utaendeshwa kwa usalama mkubwa kwani madini ya Tanzanite yana thamani kubwa. Serikali imeimarisha ulinzi wakati wa zoezi hili ili kujihadhari na watu wasio waaminifu,” alisema Shoo.
Aidha mnada huo utaiwezesha Serikali kupata mrabaha stahiki na kodi nyingine za Serikali kwa uwazi ili kuchangia pato la taifa.
Alisema kuwa minada kama hiyo pia hufanyika kwa nchi za Afrika zenye madini ya Vito kama vile Zambia (Emerald), Zimbabwe ( Almasi) pamoja na Afrika kusini ( Almasi).
Washindi wa zabuni za ununuzi wa madini ya Tanzanite wanatarajiwa kutangazwa Oktoba 15 mwaka huu mkoani Manyara.