NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa amesema atahakikisha timu hiyo inarejea kucheza staili ya kushambulia muda wote ili kuvuna mabao mengi.
Mkwasa juzi aliiongoza Yanga kuvuna ushindi wa bao 1-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Nagwanda Sijaona, Mtwara.
Kocha huyo wa mpito alichukua nafasi ya Mkongomani, Mwinyi Zahera aliyetimuliwa katikati ya wiki iliyopita.
Ushindi huo uliifanya Yanga kufikisha pointi 10, baada ya kucheza michezo mitano, ikishinda mitatu, sare mmoja na kupoteza idadi kama hiyo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkwasa alisema katika kipindi kifupi atakachokuwa na timu hiyo, atahakikisha anarudisha falsafa ya kucheza kwa kushambulia dakika zote.
Alisema kikosi hicho kimejipanga kuhakikisha kinashinda michezo yake yote ya kiporo ili kujikusanyia pointi zitakazoweka katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
“Nashukuru vijana wangu kwa kufuata maelekezo yangu na kufanikisha ushindi katika mchezo huo,japo nilikuwa na muda mchache na timu,lakini vijana walinipa ushirikiano na kufanya tulichopanga.
“Lengo ni kurudisha falsafa yetu ya kucheza kwa kushambulia, wapenzi wetu wamezoea kuiona Yanga ikimnyima raha mpinzani, tutahakikisha tunafanya hivyo ili kurudisha hadhi yetu na kupata mabao mengi zaidi,” alisema.
Mkwasa alisema anataka kukifanya kikosi hicho kuwa tishio kwa wapinzani na kurudi katika mbio za kufukuzia taji la Ligi Kuu Bara walilipoteza misimu miwili iliyopita.