Na MWANDISHI WETU
Kitendo cha Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), Dk. Athuman Kihamia kugoma kutaja gharama ambazo tume yake imekuwa ikizitumia kuendesha chaguzi za marudio ya ubunge na udiwani kimetibua nyongo za wafuatiliaji wa masuala ya siasa.
Wafuatiliaji hao wamemtaka Dk. Kihamia kutambua kuwa fedha zinazotumiwa na tume anayoiongoza si zake bali ni za umma hivyo hapaswi kufanya siri matumizi yake.
Juzi Kihamia aliwaambia waandishi wa gazeti hili kuwa kamwe hatozungumzia wala kutoa taarifa zozote za matumizi ya fedha ambazo Tume yake imekuwa ikiyafanya katika maeneo mbalimbali ikiwamo chaguzi za marudio.
Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo baada ya gazeti dada la hili la MTANZANIA Jumamosi kutaka kufahamu gharama za chini na juu ambazo NEC imekuwa ikizitumia kwa jimbo moja linalofanya uchaguzi wa ubunge na kata inayochagua diwani.
Kabla ya kutoa kauli hiyo ambayo ilichapwa kwenye gazeti la MTANZANIA toleo la jana, Kihamia alimtaka mmoja wa waandishi wa gazeti hili kati ya wawili aliozungumza nao kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwa wao ndio wazungumzaji wa suala hilo.
Mwandishi alipohoji kama utaratibu huo ni mpya alisisitiza kuwa yeye anasimamia masuala yote yanayogusa uchaguzi isipokuwa fedha hata alipoelezwa kuwa suala hilo bado linamgusa alikataa kuzungumza.
Kutokana na maelezo yake Mwandishi aliamua kuwasiliana na Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja, ambaye naye alionekana kushangazwa na swali hilo kuelekezwa kwao na zaidi akasisitiza kuwa Tume ndio wanaopaswa kuzungumzia suala hilo.
“Sisi kama Wizara ya Fedha na Mipango kazi yetu ni kutoa fedha kulingana na mipango na bajeti ambayo tumeletewa sasa sisi tutajuaje mipango yao, hilo suala halituhusu linawahusu wao ndio wanajua wanavyotumia” alisema Mwaipaja
Mwandishi alipowasiliana na Dk. Kihamia kwa mara nyingine na kumweleza kauli hiyo ya Wizara ya Fedha na Mipango, alisisitiza akisema kuwa; “Nimekwambia kamwe sitazungumzia masuala ya Fedha nukta. Wala sitataja na nimekwisha waeleza na wengine, sitaji, mimi nitazungumzia masuala yanayogusa wananchi”.
Alipoambiwa kuwa wananchi ndio wanaotamani kufahamu gharama hizo, aliendelea kusisitiza kuwa hazungumzii.
Kutokana na msimamo huo wa Dk. Kihamia, MTANZANIA Jumapili lilizungumza na Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Profesa. Mwesiga Baregu ambaye alielezea kushangazwa kwake na msimamo huo wa Mkurugenzi wa NEC.
Profesa. Baregu alisema kitendo cha Mkurugenzi wa NEC kukataa kutoa taarifa ya gharama anazozitumia kwenye chaguzi za marudio ni sawa na kutukana haki za walipa kodi ambao jasho na nguvu zao zinatumika kwa ajili ya mustakabari wa Taifa.
Alisema Mkurugezi wa NEC anatakiwa kutambua kwamba fedha zinazotumika kuendesha chaguzi ndogo sio zake bali ni wananchi na kawaida ya matumizi ya fedha za umma yanatakiwa kuwa wazi.
“Nashangaa sana kwa sababu katika matumizi ya fedha za serikali wapo maofisa ambao wanajulikana kuwa na mamlaka ya kupokea na kutumia fedha za serikali, kwenye wizara utakuta makatibu wakuu na kwenye tume mkurugenzi ndiye mwenye fungu.
“ Nimeshangaa zaidi kuona anaitupia mpira Wizara ya Fedha na Mipango, wizara haiwezi ikajua hata kidogo tume imetumia kiasi gani katika uchaguzi wa Ukonga au kwingine, bali anayejua matumizi hayo ni mkurugenzi mwenyewe wa NEC. Sasa sijui kwa nini anasema iulizwe wizara, huku ni kushindwa kuwajibika au alikuwa anaanisha nini?, kwa kweli sijamuelewa,” alisema Profesa Baregu.
Alisema msimamo huo wa Mkurugenzi wa NEC unakwenda kinyume na dhamira ya serikali ambayo imekuwa ikijinadi kufanya kazi kwa uwazi na ukweli.
Kauli kama ya Profesa Baregu ilitolewa pia na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana ambaye naye alisema Mkurugenzi wa NEC, hapaswi kufanya siri ya gharama ambazo amekuwa akizitumia kwenye chaguzi hizo.
“Hili ni jambo ambalo ni la wazi na hizi ni fedha za wananchi, kimsingi wanayo haki ya kujua tume wanatumia kiasi gani kwa uchaguzi wa marudio ya ubunge au udiwani.
“ Lakini kwa hatua nyingine tumsamehe mkurugenzi kwa sababu bado ni mgeni katika nafasi hiyo lakini angekuwa mkurugenzi kama alivyokuwa Kailima angetoa taarifa ya matumizi ya fedha kwa kila chaguzi za marudio na ninajua zitatofautiana tu sio kwamba kila chaguzi ndogo gharama ni zile zile bali hutegemea na mazingira,” alisema Dk. Bana.
Naye Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), John Mrema alisema Mkurugenzi wa NEC anapaswa kujua kwamba yupo kwenye ofisi ya umma na anawajibika kwa umma kutoa taarifa za jinsi anavyotumia kodi za Watanzania .
Alisema Chadema kinamuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) afanye ukaguzi maalumu katika fedha ambazo zinatumika katika chaguzi za marudio.
Alisema CAG akifanya ukaguzi huo anatakiwa kuueleza umma kama gharama za chaguzi za marudio zina tija kwa taifa .
Mrema alisema msimamo wa NEC wa kukataa kutaja gharama za chaguzi za marudio unaibua tafsiri kwamba inawezekana chaguzi hizo zinatumika kama uchochoro mpya wa ufisadi.
“ Haiwezekani chombo ambacho kinaendesha chaguzi za kuwapata viongozi wa umma kushindwa kusema kinatumia kiasi gani cha fedha za umma ,” alisema Mrema.