Ramadhan Hassan, Dodoma
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Paskas Muragili na aliyekuwa fundi sanifu wa mamlaka hiyo, Lemanya Benjamin, wamepandishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma makosa ya matumizi mabaya ya madaraka.
Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Emmanuel Fovo, Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Biswaro Biswaro amedai washtakiwa walitenda kosa hilo Septemba mwaka 2016.
Amedai watuhumiwa hao hawakuweka wazi maslahi yao kuhusiana na ombi la kampuni ya Glacer Investiment Co Ltd kwenye zabuni Na. LGA/020/2016-2017/W/09 yenye thamani ya Sh 86,153,956 kuhusiana na ukarabati na ujenzi wa makaravati katika barabara za Jiji la Dodoma.
Washtakiwa wako nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuweka fedha taslimu Sh milioni 23 au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 4, mwaka huu.