KIGALI, RWANDA
DIANE Rwigara ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ameshtakiwa kwa uchochezi wa uasi dhidi ya Serikali ya nchi hiyo.
Rwigara ameshtakiwa pamoja na mama yake, Adeline Rwigara na dada yake Anne Rwigara, kwa tuhuma hizo.
Mtuhumiwa huyo mkuu, Rwigara, alizuiwa kuwania nafasi ya urais wa Rwanda katika uchaguzi uliofanyika Agosti, mwaka huu.
Rais Kagame alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 99 hali iliyozua madai kuwa kulikuwa na udanganyifu, madai yaliyopingwa vikali na mamlaka ya nchi hiyo.
Mbali ya shitaka la uchochezi wa uasi, Rwigara pia ameshtakiwa kwa tuhuma za kubuni stakabadhi bandia.
Wachunguzi wanadai kuwa Adeline alivunja sheria za uchaguzi kwa kukusanya sahihi bandia kuunga mkono ugombeaji wake.