Na FERDNANDA MBAMILA -DAR ES SALAAM
MKESHA mkubwa wa kitaifa wa dua maalumu unatarajia kufanyika mwisho wa mwaka huu Desemba 31, katika mikoa zaidi ya tisa nchini.
Mkesha huo unatarajia kufanyika katika viwanja tofauti tofauti ambapo Dar es Salaam utafanyika Uwanja wa Uhuru, (Dodoma) Uwanja wa Jamhuri, (Kilimanjaro) Uwanja wa Mahakama ya Mwika Kiruweni, (Iringa) Uwanja wa Samora, (Mwanza) Uwanja wa CCM Kirumba, (Ruvuma) Uwanja wa Majimaji, (Singida) Uwanja wa Mtu Mbili, (Morogoro) Uwanja wa Kilosa na Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Askofu Dk. Godfrey Malassy wa Kanisa la Tanzania Fellowship, alisema 2017 ni mwaka wa pekee zaidi katika Taifa la Tanzania kufuatia matendo makuu ya Mungu aliyotutendea Watanzania hasa kutokana na azi njema inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.
Alisema Rais ameonyesha mwanga na dira katika usimamizi wa rasilimali zote za nchi kwa kipindi kifupi tu, lengo ni kujenga Tanzania iliyo imara na yenye maendeleo.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa amesikia dua zetu Watanzania na ulimwengu mzima ni mashahidi wa Tanzania mpya na yenye amani na utulivu, inayotoa fursa kwa wananchi wote kufanya kazi kwa bidii na kujenga uchumi imara,” alisema Askofu Malassy.
Alisema 2017 ni mwaka wa kipekee kwa Taifa hivyo ni fursa adimu kwa Watanzania kukusanyika nchi nzima kwa sauti moja na kusimama pamoja usiku wa Desemba 31 kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuvusha salama 2017 kwa amani na utulivu, kuomba dua maalumu kuupokea mwaka 2018 kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu.