Na Othman Miraji
KUNA kirai kwa lugha ya Kijerumani ambacho kinatafsirika kijuujuu kwa Kiswahili kama hivi: Ilimradi tu ufikie lengo, hata ikibidi kukanyaga lundo la maiti mbele yako.
Mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi, aliyeuliwa Oktoba 2, mwaka huu ndani ya Jengo la Ubalozi Mdogo wa nchi yake mjini Istanbul, Uturuki, alitajwa na wakuu wa nchi yake kuwa ni adui wa nchi.
Licha ya hayo, Marekani haijali, imesema itaendelea kufanya biashara na Riyadh na uhusiano baina ya nchi hizo mbili utaendelea kama ilivyozoeleka mnamo miaka iliopita. Inasaidia nini kupiga sana kelele juu ya mauaji ambayo yameshatokea? Cha kusikitisha ni kwamba si Marekani peke yake inayofikiri namna hivyo.
Rais Donald Trump wa Marekani alisema kwamba Marekani inakusudia kubakia mshirika mkakamavu wa Saudi Arabia ili kuhakikisha maslaha ya nchi yetu, Israel na washirika wote katika eneo hilo. Ni lengo letu kubwa kuitokomeza hatari ya ugaidi duniani kote.
Watu duniani walibakia wanaulizana: Je, vipi kuhusu haki za binadamu na mapambano dhidi ya udikteta? Kupata kandarasi za kibiashara ni muhimu zaidi kwa Trump kuliko haki za binadamu. Yeye yuko tayari kuwaridhia kwa vyovyote watawala wa mabavu na madikteta na kuridhia mauaji wanayoyafanya ikiwa tu wataipatia Marekani fedha.
Itakumbukwa kwamba wakati wa kampeni za uchaguzi wa kuwania urais, Trump aliwahi kuitaja Saudi Arabia kuwa ni chimbuko la ugaidi. Lakini pale Wasaudi walipotishia kuondosha fedha zao na uwekezaji kutoka Marekani, Trump aliacha kuendelea kutamka maneno hayo na akajifanya anazisahau pia itikadi kali za madhehebu ya Wahhabi wa Saudi Arabia zinazoihatarisha Israel. Alijifanya hamnazo na kusahau kwamba Wasaudi wengi ndio walioshiriki katika mashambulio ya Septemba 11, 2001 huko Marekani. Siasa ya Trump ni ya ndumila kuwili.
Kwa Rais Trump hoja yake, pale anapouangalia Mkasa wa Khashoggi na kujaribu kuupatia suluhisho la kidiplomasia, ni kwamba mbele kabisa yaangaliwe, kuliko chochote kingine, maslahi ya Marekani- Marekani Kwanza. Mkuu huyo wa Washington ametangaza wazi vita dhidi ya watu wote wanaoweka mbele kabisa uadilifu na wanaoamini kwamba inabidi Saudi Arabia sasa iadhibiwe na iwekewe vikwazo. Na hiyo tu kwa vile Mrithi wa Mfalme wa nchi hiyo, Mohammed bin Salman, aliamrisha kuuliwa kikatili ndani ya Ubalozi Mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul mwandishi wa habari aliye mpinzani wa serikali.
Trump hajawa na kigugumizi. Alitamka wazi pale alipozungumza juu ya kuuliwa Jamal Khashoggi: kwake ni sawa kabisa kama Khashoggi aliuliwa kutokana na amri iliyotolewa na Mwanamfalme Mohammed bin Salman, au kama Mwanamfalme huyo hajawa na taarifa kabla ya kufanyika mauaji hayo.
Trump aliahidi kwamba Marekani itaendelea kusimama upande wa Saudi Arabia, hivyo ameonesha wazi kwamba nchi yake inavutiwa zaidi na fedha, tulipokuwa watoto wadogo tukiita Njenje Hapa ni suala la ngwenje itakazofaidi Marekani katika kufanya biashara na Saudi Arabia.
Kwa Trump ilimradi njenje zinaingia mfukoni mwa Marekani, yeye hajali, ni sawa kwake yale yanayotendwa na watawala wa Riyadh. Katika taarifa yake Trump hata mara moja hakujaribu kuificha risala yake hii. Taarifa yake hiyo inaweza tu kuangaliwa na watawala wa Saudi Arabia kuwa ni ruksa wazi kwa yale wanayoyafanya.
Lakini kuna hatari. Maneno hayo yanayotamkwa na Trump huenda yataweza kutamkwa pia na Ujerumani, Italy au Ufaransa. Saudi Arabia ni nchi muhimu kabisa inayotoa mafuta baada ya Marekani. Ni nchi iliyo tajiri sana, mataifa mengi yanategemea mafuta ya nchi hiyo ya Kiarabu na hayathubutu kuikaripia vikali.
Watu wasiojali uadilifu wanauliza: kwanini dunia inajali sana juu ya mauaji yaliyoamrishwa yafanywe na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia wakati kuna uhondo mkubwa wa biashara yenye kugharimu matrilioni ya njenje?
Mkasa huu wa Khashoggi umewatia moyo madikteta na watawala wa mabavu duniani kote. Sasa wanahisi wana hakika wanapoziona haki za binadamu na maendeleo ya kiuchumi si mambo yanayotiliwa maanani ilimradi suala la viwanda vya kutengeneza silaha huko Marekani vinapata kandarasi. Kwa hivyo, tawala za mabavu zimepata sababu za kuwakandamiza raia wao na pia kuwatuma wauaji nje ya nchi zao kuwaandama wapinzani.
Mwenyewe Trump, bila ya haya wala kupepesa macho, alizitaja tarakimu na kupima katika mizani baina ya mabilioni ya madola hayo ya Kimarekani na uadilifu wa kuililia roho ya Khashoggi. Mkuu huyo wa Marekani alihoji kwamba fedha hizo katika mezani ni nzito zaidi kuliko maisha ya binadamu Khashoggi. Imetajwa kwamba Saudi Arabia itawekeza Dola bilioni 150 katika ufundi wa kutengeneza silaha huko Marekani na kuna silaha zitakazonunuliwa zinazogharimu Dola bilioni 450.
Pia kuna mikataba ya uwekezaji na nchi hiyo ya Ghuba, ambayo, kwa mujibu wa Trump, itasababisha kuwapo maelfu ya nafasi za kazi huko Marekani. Kutokana na ripoti za Ikulu ya Marekani nafasi mpya za kazi 40,000 zitapatikana na jambo hilo si la kukisia juu juu tu. Mabilioni ya dola yanalinganishwa na roho ya mwanadamu, jambo la kuhuzunisha. Hatusomi katika vitabu vitakatifu kwamba kuua roho moja ni kama kuua wanadamu wote?
Cha kusikitisha zaidi ni kwamba Trump ameikumbatia hoja ya wakuu wa Saudi Arabia, kuifanya hoja hiyo ni yake, kwamba Khashoggi alikuwa adui wa dola hiyo. Kwa hivyo, anasema waziwazi bila ya kuficha, kwamba ni sawa na ni haki auliwe mtu yeyote anayeupinga utawala wa Ufalme wa Saudi Arabia. Tutegemee nini tena pale Trump anapoviangalia vyombo vingi vya habari kuwa ni maadui wa umma?
Dunia hivi sasa imeshazoea kumuona Trump akitamba na ushabiki wake wa Marekani Kwanza. Kila wakati yuko tayari anayavuruga bila ya kujali mapatano ya kimataifa na vipimo vya kimaadili. Sasa amekwenda mbali zaidi. Je, Mrithi wa Mfalme wa Saudi Arabia aachiliwe aue watu kikatili kama apendavyo? Na tena hasa kisa hiki chenyewe kinamuhusu mwandishi wa habari na tena zaidi ni kwamba mwandishi huyo analifanyia kazi gazeti la Kimarekani?
Ukweli ni kwamba Marekani imewakumbatia madikteta zaidi kuliko ilivyo Saudi Arabia. Hakuwahi kutokea Rais wa Marekani kama alivyo Trump aliyefungamanisha zaidi, tena waziwazi, maslahi yake na yale ya madikteta hao. Hali hiyo iliyo wazi inaiharibu heshima ya dola hilo kuu ambako Rais wa nchi ni mtu muhimu sana. Na hapa halihusiki suala la kuibakisha Marekani iwe Nambari Moja Duniani, kama anavyopenda Trump kusema. Yaonesha anachotafuta mwanasiasa huyo ni kuwa mvumbuzi wa siasa isiyojali huruma katika kukimbilia kujipatia maslahi ya kibinafsi.
Marekani kutaka kubakia Nambari Moja Duniani inabidi ijivalishe pia joho la uadilifu na Trump hana joho hilo. Yeye anaendesha tu siasa ya kutafuta umaarufu miongoni mwa wapiga kura, ya kupigiwa makofi, bila ya kujali kupotea heshima ya Marekani kama Taifa lenye kuheshimu utu na ubinadamu. Na pale wanasiasa na serikali zinakuwa wa mwanzo kutoziamini taasisi zilizoko pamoja na changamoto zilizoko mbele ya taasisi hizo, kuna hatari ya raia kufuata mifano yao na taasisi hizo kutojaliwa mara mbili zaidi.