27.7 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Misamiati ya kale yarejea kusafisha mapungufu ya utawala

HILAL K SUED

JAMII ya nchi hii imeshuhudia misamiati na kauli mbiu nyingi sana katika kuelezea sera na kusimamia maendeleo ingawa mwisho wa siku maendeleo bado, kwa maana wananchi wengi bado ni masikini.

Nakubali yapo maendeleo katika maeneo kadhaa (maeneo ya ki-sekta) kama vile miundombinu, mawasiliano ya simu za mikononi na maeneo mengine machache, lakini narudia bado hali za watu wengi ni duni sana hasa kule vijijini.

Misamiati hiyo iliyopita, hasa baada ya kuasisiwa kwa Azimio la Arusha na itikadi ya Ujamaa chini ya uongozi wa Awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere – kama vile mabepari, mabeberu, ukoloni mamboleo, makabaila, makupe na mabwanyenye ilizikwa mwaka 1992 kule Zanzibar ingawa wale waliohusishwa nayo na/au warithi wao bado wapo, kivingine na sasa wanatambuliwa kwa misamiati mengine.

Ukweli ni kwamba mabwenyenye na mawakala wao wapo wengi tu. Kwenye utalii wamejaa. Kwenye masuala ya umeme wamejaa na ndiyo waliotuingiza chaka kuanzia enzi za Mwinyi na ni katika nyakati hizi ndipo wameweza kudhibitiwa.


Kwenye upigaji wa fedha za benki kuu wamejaa. Ni wengi sana na wanakula kutokana na matumizi ya elimu yao na kukingwa na wale waliowaweka pale. ‘Wakingaji’ ni wakubwa katika utawala na wanasiasa wa chama kinachotawala kwa zaidi ya nusu karne sasa. Halafu mtu anapata ubavu kusema chama hicho kinaweza kuondoka madarakani kirahisi.

Kwa ujumla tangu baada ya uhuru mapema miaka ya 60 watu hawa walikuwa wanalaumiwa kwa kila kitu kilichokuwa kinakwenda sivyo ndivyo nchini na walifanywa mbuzi wa kafara kuelezea sababu za kukosekana/kurudisha nyuma maendeleo, wizi wa mali za umma na kadhalika.

Siku hizi tuna wajasiriamali, wawekezaji, wadau wa kimaendeleo, wafadhili na kubwa ya yote, utandawazi. Kilichobaki sasa ni kuyafutilia mbali hayo maneno yale ya kizamani kwenye kamusi zetu za Kiswahili.

Lakini huwezi kufuta au kubadilisha historia ili kukwepa madhambi. Watu wanaotaka kufuta historia huwa wana malengo yaliyo maovu (sinister motives), kusafisha maovu yaliyotokea.

Kujaribu kusafisha maovu yaliyotokea katika historia ya nchi si kitu muafaka kwa sababu inaviacha vizazi vijazo bila kumbukumbu sahihi ya mambo yaliyotokea kwa ajili ya kujifunza ili kutorudia makosa.

Kule Ujerumani hadi leo kunafundishwa historia ya dikteta wao Hitler aliyesababisha janga kubwa duniani, Vita ya Pili ya Dunia ambayo ilisababisha vifo takriban milioni 50 duniani kote. Wanafundishwa ili wajifunze makosa ya mababu zao ili yasirudiwe.

Tujikite hapa hapa kwetu. Kuna madai kwamba eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam ambalo katika miaka ya 60/70 lilikuwa ni mashamba ya mikorosho lilijengwa kupitia fedha zilizotokana na ufisadi, yaani utafunaji wa fedha za mashirika ya umma uliofanywa na wakubwa wa mashirika hayo hadi yakaja kufilisika. Fedha hizo haramu ndiyo zilijenga makasri mengi katika eneo hilo.

Ndiyo maana hadi leo hii utaona kwamba pamoja na majengo ya anasa ya eneo hilo, barabara na miundombinu mingine bado ni duni sana, ishara kwamba wamiliki wa majengo hayo wana fedha kuliko serikali.

Lakini ni wakubwa wangapi wa mashirika hayo waliwajibishwa kwa ufisadi huo? Kama wapo ni wachache sana. Lakini tusisahau pia kwamba mashirika hayo ya umma yalikamuliwa na wajanja katika awamu mbili tofauti, kwanza ni awamu ile ya yalipofilisiwa na wachache na pili ni pale yalipokuwa yakibinafsishwa baada ya Azimio la Zanzibar.

Bado hakuna tathimini rasmi iliyofanywa kuonyesha nchi ilipata hasara na kurudi nyuma kimaendeleo kwa kiasi gani kutokana na matukio hayo mawili. Na kwa kuwa uwajibikaji ulikuwa ni kidogo sana, basi mambo yakaendelea na yanaendelea pengine si kwa namna ile.

Hivyo basi wale waliokuwa wanawatuhumu mabwanyenye, mabepari, makabaila na mabeberu kwa uduni wetu bila shaka walijikuta wanasutwa.

Ni sisi wenyewe ndiyo wakulaumiwa hususan wachache miongoni mwetu waliopewa dhamana katika kusimamia rasilimali za nchi.

Hivi sasa baadhi ya misamiati hiyo imeanza kurejeshwa tena katika madhumuni yale yale ya kusukumiana lawama yanapotokea mapungufu katika utendaji wa utawala.

Sasa hivi tunazisikia kauli kama vile “kuna watu humu nchini wakishirikiana na mabwanyenye wa kimataifa wamedhamiria kumkwamisha Rais Magufuli katika jitihada zake za kuokoa rasilimali za nchi.”

Chukua suala la madini kwa mfano. Pamoja na jitihada nyingi za Rais Magufuli kutaka kuonyesha kwamba ni watu wa nje ndiyo walikuwa wanatunyonya kupitia madini yetu lakini ni ukweli pia walifanya hivyo kwa msaada wa baadhi ya watawala wetu kupitia mikataba ya ovyo.

Labda mtu atuthibitishie kwamba wale waliokuwa katika dhamana za kutia saini mikataba ya uchimbaji madini walifanya hivyo huku wamewekewa bastola vichwani mwao. Na hata wale wachache waliotajwa katika kufanikisha unyonywaji huo katika sekta ya madini hawajafanywa chochote – mbali na kutajwa tu.

Kuna mambo mengi yasiyoeleweka kuhusu vita nzima dhidi ya ufisadi katika awamu mbalimbali za utawala na si vigumu kupata picha kwamba hakuna umakini wowote katika vita nzima katika awamu zote.

Kuanzia miongo ya karibuni tuna mafisadi ambao wamegoma kujulikana, achilia mbali kushughulikiwa kwa majibu wa sheria. Mara kadha hawa hutajwa tu hadharani na mara nyingine si kwa majina, bali kwa matukio ya ufisadi walioufanya watu wakajua ni akina nani, ingawa mwisho wa siku hatuoni kinachofanyika dhidi yao.

Wengine baada ya kubainika kufanya ufisadi huambiwa warudishe fedha walizojipatia kwa njia haramu ili yaishe. Huu ni mfumo mpya wa usimamizi wa sheria, mbali na ule wa kawaida uliobuniwa wakati wa kashfa ya EPA miaka kumi iliyopita.

Watu walihoji kwanini mfumo huo wa sheria usitumike kwa watu wengine pia waliohusika kuiba fedha za umma? Hawa ni pamoja na wafungwa walio gerezani walioiba fedha za umma na kuhukumiwa vifungo na ambao bila shaka wengi wao wako tayari kurudisha fedha ili waondokane na adhabu ya kukaa lupango.

Lakini kuna hili lisiloeleweka kabisa: Katika wizi wa kashfa ya Escrow kuna wengine, hususan mmoja aliyetangaza amerudisha mamilioni TRA ingawa ilidaiwa TRA iliyakataa marejesho hayo ya fedha.

Haya mambo mtu anaweza kudhani ni kichekesho, lakini kwa watu makini ni ishara ya mambo ya ajabu yanayotokea katika ‘sekta’ nzima ya ufisadi na mapungufu makubwa kwa utawala kuyasimamia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles