30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

‘MIRADI YA MAENDELEO IKABIDHIWE HALMASHAURI’

Na MWANDISHI WETU -BAGAMOYO

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola, ameshauri miradi ya maendeleo inayohusiana na utunzaji mazingira isimamiwe na halmashauri husika ili kuepuka gharama na kupatikana ufanisi.

Hayo aliyasema jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na maofisa wa halmashauri ya wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo, Majid Mwanga, kuhusiana na kuchelewa kwa mradi wa maji safi uliopangwa kukamilika Januari mwakani, lakini hadi sasa hauna dalili ya kuanza.

“Nasikitika fedha zipo lakini mradi haujaanza, sababu ni moja tu halmashauri haijashirikishwa ipasavyo matokeo yake tutaanza kulaumiana sisi watu wa Serikali.

“Miradi mikubwa namna hii lazima halmashauri zishirikishwe ili watoe wataalamu na kushauri sehemu gani kutiliwe mkazo kwa sababu wao ndio wanaojua matatizo ya wananchi,” alisema Lugola.

Naibu waziri huyo alifanya ziara wilayani hapa ili kukutana na wasimamizi wa mradi wa maji safi unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wenye lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na athari ya vyanzo vya maji kwa wakazi wa pembezoni mwa bahari kuingia chumvi.

Hata hivyo, mradi huo unaogharimu Sh milioni 912 ulianza kufanyiwa tathmini tangu mwaka 2012 na kuanza utekelezaji Januari 2015, ukiwa na lengo la kuchimba visima 17 na kujenga matanki ya kuhifadhi maji ya mvua katika taasisi tano za Serikali, hadi sasa hakuna kilichofanyika huku malengo ya mradi ni kukamilika Februari mwaka 2018.

“Huu ni miongoni mwa miradi mibovu niliyowahi kushuhudia, taarifa inaonyesha mkandarasi alileta vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji tangu Septemba mwaka huu, lakini ujenzi haujaanza naomba kabla ya wiki hii kuisha niletewe taarifa kamili za fedha na ufuatiliaji mradi nini kimetokea.

“Wananchi hawataki kusikia mambo ya michakato wanataka kuona maji yanatoka, lakini pia kuna shule hapa za msingi na sekondari zipo ndani ya mradi, wanafunzi hawa wanahitaji maji safi mradi huu ni wa siku nyingi ufike mwisho,” alisema Lugola.

Awali akitoa taarifa k ya mradi huo, Mratibu Mradi Wilaya, Mhandisi Jason Niraphael, alisema lengo la mradi huo ni kuiwezesha jamii ya Pwani kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wanaokadiriwa kufikia 10,000 wanaoishi kando ya Bahari ya Hindi katika Wilaya ya Bagamoyo.

“Kwa kuzingatia tathmini iliyofanyika mwaka 2012, ilikubalika ujenzi wa visima 17 na matanki ya kuhifadhia maji ya mvua katika taasisi tano.

“Mkandarasi wa ujenzi wa matanki hayo ameshaleta baadhi ya vifaa eneo la kazi na Taasisi ya CC FORUM na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanaendesha mafunzo kwa wadau mbalimbali kuhusiana na mradi huo,” alisema Jason.

Wakati akiendelea kutoa taarifa hiyo, alisema kutokana na sababu zisizozuilika visima vimepunga kutoka 17 hadi 10 na matanki ya kuhifadhia maji ya mvua yameshuka kutoka matano hadi mawili ambayo yatawekwa katika shule za Sekondari Kingani na Matipwili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles