NA MWANDISHI WETU,
GEORGE Lwandamina amevutiwa kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga, baada ya kuahidiwa mshahara wa dola za Marekani 18,000 (shilingi 38,448,500) ikiwemo marupurupu endapo atashinda ligi na kufanya vyema kwenye michuano ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Zambia, Lwandamina ambaye anatajwa kuchukua mikoba ya Hans van der Pluijm aliyejiuzulu mapema wiki hii, aliamua kuitema Zesco United baada ya klabu hiyo kushindwa kumpa mkataba mpya au kuboresha ule uliopo.
Taarifa hizo zinaendelea kusema Lwandamina aliyeiongoza Zesco United kufika hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu, alikua anapokea mshahara wa dola za Marekani 3,500 (shilingi 7,476,110).
“Lwandamina ataondoka baada ya msimu huu wa Ligi Kuu Zambia kumalizika baada ya kufikia makubaliano na Yanga, ukizingatia Zesco wameshindwa kumpa mkataba mpya au kuboresha wa awali,” ilisema taarifa hiyo.
Kuondoka kwa Lwandamina anayetajwa miongoni mwa makocha bora Zambia kwa sasa, kumefungua milango kwa wachezaji nyota wa Zesco United kuihama timu hiyo.
Wachezaji wanaotajwa kuondoka Zesco United na huenda wakamfuata Lwandamina ni mshambuliaji Mkenya, Jesse Were, beki raia wa Kenya, David Odhiambo ‘Calabar’ na kiungo mchezeshaji, Cletus Chama.
Were amekua akihusishwa na Bidvest Wits ya Afrika Kusini, lakini ni moja wa washambuliaji wanaotajwa kuwa kipenzi cha Lwandamina kama ilivyo kiungo Chama.