HADIJA OMARY, LINDI
Kampuni ya mafuta na gesi (Equinor Tanzania), imetoa kiasi cha Sh milioni 20 kwa Hospitali ya CCBRT kwa ajili ya kuwafanyia upasuaji wanawake 80 wanaougua fistula katika Mkoa wa Lindi.
Akitoa salamu za kampuni, Mkurugenzi mkazi wa kampuni hiyo Dk Mette Ottoy amesema mpango huo ya matibabu kwa wagongwa wa fistula kwa Mkoa huo utaendeshwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inafanyika mwaka huu na awamu ya pili itaendeshwa mwakani.
Naye Mkurugenzi wa CCBRT Dk Blenda Msangi amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili akinamama wengi wanaougua fistula katika maeneo yaliyomengi ni kushindwa gharama za matibabu pamoja na gharama za usafiri kutoka maeneo wanayoishi mpaka katika vituo vya kutolea huduma, hivyo wanawake wengi hukosa kupatiwa matibabu ya haraka kwa kushindwa kumudu gharama hizo.
“Takwimu zinaonyesha zaidi wanawake 3,000 wa kitanzania wanapata tatizo la Fistula kila mwaka hali ambayo huwaacha akina mama hawa katia mazingira magumu huku mkojo na kinyesi vikiwa vinawatoka bila udhibiti lakini ni wanawake wachache ambao wanaenda kupatiwa matibabu,” amesema.
“Changamoto nyingine ni imani potofu ambapo wanawake wengi hudhani ugonjwa wa kutokwa na mkojo ama kinyesi bila udhibiti ni kunatokana na mama wakati wa ujauzito wake kushiriki kimapenzi na wanaume wengi ama kulogwa jambo hilo huwafanya akinamama wengi kuchelewa kuwahi katika vituo vya kutolea huduma kwa kuona aibu,” amesema.
Kwa upande wake kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dk Stellha Kihombo amesema sababu zinazopelekea mwanamke kupatwa na tatizo la fistula ni kukosa huduma bora ya afya wakati wa kujifungua, ikiwa sambambana na kuchelewa kufika kwa wakati kituo cha Afya.