Johanes Respichius, Dar es Salaam |
Kamati ya fedha ya Manispaa Ubungo jijini Dar es Salaam, imemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuwasimamisha kazi mameneja wa masoko sita na watumishi watatu kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha Sh milioni 293.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Juni 8, Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob, amesema hatua hiyo ni kutoka na ripoti ya Mkaguzi wa Manispaa ya uchunguzi wa ukusanyaji wa mapato katika masoko 16 ya wilaya hiyo.
Aliwataja wanaotakiwa kusimamishwa na na masoko yao kwenye mabano kuwa ni Obote Etta (Soko la Ndizi Mabibo), Grayson Sebastian (Simu 2000), Frida Michael (Shekilango), Edwin Mugila (Mabibo) na Bakari Mshanga (Sinza) kwa upande wa watumishi wa Manispaa ni Mweka Hazina, Ofisa Mapato na Msimamizi wa Mfumo.
“Baada kutoridhishwa na taarifa ya mapato yatokanayo na masoko, Mkaguzi wa Manispaa ilibidi akachunguze kilichosababisha makusanyo kushuka hadi milioni 716.
“Ripoti yake imebaini ubadhirifu wa zaidi Sh milioni 293 ambapo mapato halali yanayoonekana kwenye mfumo ni zaidi ya Sh bilioni moja lakini baada ya kuwabana wamerejesha kiasi cha Sh milioni 139,” amesema Jacob.