28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

‘Mikebe’ yawafanya wanaume watelekeze wake, watoto Ruangwa



TABIA ya baadhi ya wanaume wanapopata vipato kuwatelekeza  wake zao na
kukimbilia kwa wanawake wa nje, maarufu kwa jina la ‘Mikebe’  imeshamiri
katika kata za Ruangwa na Nachingwea, wilayani hapa, mkoani Lindi.

Hali hiyo huwafanya watoto kukosa haki zao za msingi ikiwamo malezi bora kwa sababu wahusika wanaofanya vitendo hivyo hushindwa kutimiza majukumu yao katika familia na kuiacha ikihangaika.

Utelekezaji wa familia ni kati ya vitendo vya ukatili vilivyoshamiri
wilayani humo, na kusababisha watoto kukosa mahitaji muhimu hivyo,
kuchangia ongezeko la utoro kwa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi kwa kukosa mahitaji muhimu kama sare za shule, viatu na madaftari.

Utafiti wa kihabari uliofanywa wilayani hapa na mwandishi wa makala
haya kwa msaada wa Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA),
ulibaini baadhi ya wanaume hutelekeza familia zao baada ya kupata
vipato vya biashara au mavuno na kwenda kwa vimada ambao hufahamika
kwa jina maarufu la ‘mikebe’.

Aidha, vipato vya wakazi wa eneo hilo vinatokana na shughuli
mbalimbali kama kufyatua matofali, kuponda kokoto, mauzo ya mazao ya
korosho, mbaazi na mengineyo.

Hata hivyo, utafiti umebaini kuwa baadhi yao hukimbia familia zao
kutokana na hali ngumu ya kipato.
Mkazi wa Kijiji cha Gogovivu, Kata ya Ruangwa, Hatia Mohamed, ni miongoni mwa waathirika aliyejikuta katika wakati mgumu kwa kuachwa na mumewe baada ya kujifungua mapacha.

Hatia, ambaye kwa sasa ana watoto watatu baada ya kujifungua mapacha
hao, ameachwa bila msaada wowote kutoka kwa mzazi mwenzake anayedaiwa kumtelekeza na kwenda kuishi na kimada.

Kutokana na hali hiyo, aliamua kuwabeba watoto wake na kuwapeleka Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Likangara, kutoa
malalamiko ili mzazi mwenzake aitwe na kutoa maelezo kuhusu tuhuma
zinazomkabili.

Akisimulia mkasa huo, anasema alikuwa akiishi na mumewe kwa amani
tangu enzi za urafiki, uchumba hadi walipofanikiwa kupata mtoto wao wa
kwanza.

“Nina takribani zaidi ya miaka minne hivi tangu nilipoolewa na kuishi
na huyu bwana (Mohamed), lakini alibadilika mara nilipojifungua
watoto hawa mapacha, Said na Rajab Mohamed.

Anasema mumewe alipopata fedha zilizotokana na shughuli
zake za kufyatua matofali, alianza kubadili ratiba ya kurudi nyumbani.
Anasimulia kuwa mumewe alianza kurudi nyumbani usiku mwingi tofauti na alivyokuwa awali.

Nilipojaribu kumuuliza kuhusu kuchelewa kwake na kutoacha fedha za
matumizi kwa waoto, alinijibu kwamba yeye si mume wake…nikaamua
kunyamaza tu,” anasema na kulalamika:
“Suala lingine lililonifanya niende kwa mtendaji ni baada ya yeye kushindwa hata kuwanunulia watoto nguo za kuendea kliniki.”

Mama mzazi azungumza
Akizungumza nyumbani kwake katika mtaa wa Gogovivu, Kitongoji cha
Msikitini, Kata ya Ruangwa, mama wa Hatia, Hadija Issa, anasema mara
nyingi amekuwa akipokea malalamiko ya mwanawe kuachiwa jukumu la kulea
watoto, lakini alikuwa hafuatilii.

“Niliogopa kwa sababu nikifuatilia nitaambiwa nina kimbelembele na
kwamba huo ni ugomvi wa watoto, hivyo hata ushauri niliacha kuwapa kwa
sababu mimi nitaonekena mtata,” anasema Hadija.

Baba mlezi wa Mohamed
Baba mlezi wa Mohamed alijiyejitambulisha kwa jina moja la Abiola,
maarufu Mpasuambao, anasema kijana wake bado ana nguvu na uwezo wa
kuwalea watoto wake, lakini ana tamaa ya kupenda wanawake wa nje.

“Mudi ni mtu wa kupenda ‘mikebe’ yaani vimada ila cha msingi mimi
nitamweleza kuhusu hili atakaporudi kwenye shughuli zake hivyo, kama
mnaweza kuwasaidia hawa watoto wasaidieni tu,” anasema baba huyo.

Mgogoro kama huo, pia umeikumba familia ya Abdallah Musa na
mkewe Samoe Mangula, ambao walifika katika ofisi ya Mtendaji wa Kijiji
cha Likangara ili kusuluhishwa na baadaye wahusika walikubaliana kugawana
mali.

Samoe anasema alifikia hatua hiyo baada ya kuona mumewe hana mwelekeo
wa maisha na kuamua kujihusisha na biashara ya ususi wa nywele ili
aweze kujipatia kipato cha kuendesha maisha yake na mwanawe.

“Nimekuwa nikimhudumia huyu mwanamume kuanzia chakula, usafi kila kitu kwa muda zaidi ya miezi sita haachi hata senti mezani,” anasema Somoe.

“Yaani nilikuwa kama ndio niliyeoa, sasa nimechoka nimetafakari
kwa muda wa miaka sita tangu niishi naye sijaona mabadiliko.
Abdallah Musa, ambaye shughuli zake ni kuponda kokoto, anakiri
kusaidiwa na mkewe, lakini anasema ugumu wa maisha kwa upande wake
ndiyo umesababisha yote hayo.

Hata hivyo, anasema mkewe hamheshimu kwa sababu wakati mwingine anaweza
kutoka kwenda kwenye shughuli bila kumuaga.
“Kwa kifupi, mimi sina shughuli rasmi ya kuniingizia kipato hivyo,
nimekaa nikaona kwa kuwa mwanamke huyu ameamua kuachana na mimi,
basi nilirudishiwe fedha yangu ya mahari. Tulikubaliana nilipe Sh 300,000 nikatoa
Sh 100,000; anirudishie hizo fedha zangu,” anasema Musa.

Kauli ya Mtendaji wa Kijiji
Mtendaji wa Kijiji cha Likangara, Magreth John, anakiri kupokea
malalamiko ya wanafamilia hao na kwamba bado wanashughulikia suala hilo.

Takwimu za Jeshi la Polisi

Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi, kupitia Dawati
la Jinsia zinaonesha kuwa jumla ya kesi 10 za kutelekeza familia zimeripotiwa
katika vituo mbalimbali vya polisi mkoani hapo kwa kipindi cha mwaka
jana.
Mkuu wa dawati hilo, WP Frida Mayala, anasema kati ya kesi hizo, mbili
wahusika walitiwa hatiani kwa mujibu wa sheria na nyingine bado
zinaendelea kusikilizwa mahakamani.
“Kesi nyingi za kutelekeza familia, wahusika huwa wanamalizana wenyewe nyumbani, hata hizo
zinazofika kituoni nyingi haziendelei baada ya kukaa wenyewe ngazi ya
familia kisha kukubaliana,” anasema Frida.

Taasisi isiyo ya Serikali inayojihusisha na utoaji wa elimu ya afya na
ujasiriamali kwa watoto na wanawake nchini (Kiwohede), imejitolea
kuwapatia elimu hiyo wasichana zaidi ya 600, wenye umri kati ya miaka
14 hadi 25, waliopata mimba katika umri mdogo na kisha kutelekezwa na
waume zao wilayani Ruangwa.

Mnufaika na elimu hiyo ni Husna Mwishehe, aliyeolewa na kupata mimba
akiwa na umri wa miaka 14, ambapo kijana aliyempa ujauzito, Adam
Khamis, alimtelekeza baada ya miaka mitatu alipojifungua.

“Nashukuru Kiwohede kwa kunipatia elimu ya kujitambua na
ujasiriamali, tumeahidiwa kupewa mikopo kupitia vikundi vyetu tulivyonavyo, tutakuwa tunanunua malighafi na kutengeneza bidhaa kisha
tutauza na kukopesha wateja ili tupate fedha za kuendesha maisha yetu
na watoto,” anasema Husna.

Mjumbe wa kamati zilizoundwa na TAMWA, na Mwanasheria Msaidizi, Amri
Libaba, anasema wanapoletewa malalamiko ya wanandoa baada ya
kuwasikiliza hutoa uamuzi wa kugawana mali walizochuma pamoja kama
wakiridhia.

“Wananchi wengi huku hawana elimu ya sheria hivyo, tunaendelea kuwapa
elimu ili watambue haki zao za msingi, na endapo wasipoelewana
tunawapa barua waende ngazi ya juu ambayo ni polisi ama mahakamani,”
anasema Libaba.
Kwa mujibu wa sensa ya 2012, Tanzania ina jumla ya vijana 625,000 na
robo tatu ya wasichana huzaa kabla ya kufikia umri wa miaka 20. Mkoa
wa Shinyanga unaongoza kwa asilimia 59 ya wasichana walio na umri kati
ya miaka 15 -19 kuolewa mapema.

Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wilayani hapo, Wamoja Mwinyimadi, anasema
malalamiko ya kutelekeza familia ni mengi ambapo mara nyingi hutokea kipindi
cha mavuno ya korosho au mbaazi.
Wamoja anasema kwa kipindi cha Juni, mwaka huu, wamepokea malalamiko kati ya 10 -15 ya wanaume kukimbia familia zao na kutelekeza
watoto.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dodoma, iliyopo Kata ya Nachingwea,
Hamis Nakase, anasema kitendo cha wanafamilia kutengana huathiri maendeleo ya elimu kwa watoto.

“Tatizo la utoro si kubwa, kinachotokea mzazi akitengana na
mwezake wakati mwingine utakuta anamhamishia mwanawe shule iliyo karibu na alikohamia, ila hawaachi shule kabisa kwa sababu elimu
ni bure,” anasema Mwalimu Nakase.

Viongozi wa dini
Sheikh Abdallah Kaveje, kutoka Msikiti wa Qadiria Wilayani hapo
anasema kuna msimu wa watu kufunga ndoa ambao ni Septemba hadi Desemba
kila mwaka.
Anasema kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu,
amepokea malalamiko na migogoro kisha kusuluhisha wanandoa watano kati
ya ndoa saba alizofungisha katika msimu uliopita.

“Malalamiko mengi ninayopokea ni ya wanawake wakihitaji kupewa talaka
na kutaka mgawanyo wa mali walizochuma na mumewe,” anasema.
Kaveje anatoa wito kwa wanandoa kuhakikisha wanaheshimu ndoa kwa
sababu ni sehemu ya ibada na kwamba viongozi wa dini na siasa
watoe elimu kwa jamii kuhusu maisha na ndoa.

Nini kifanyike
Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya
Ruangwa, Joseph Mkirikiti, anasema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kuoa kwa kufuata taratibu za dini zao na kuepuka migogoro.

“Kuna kesi nyingi hapa mfano mojawapo niliyowahi kuisikia ni ya mwanamke aliyeolewa na bila aibu akathubutu kumwambia mumewe kwamba
amechoka kuishi naye hivyo anaomba waachane.

Anasema idadi kubwa ya wanawake ndio hawaheshimu ndoa, imekuwa ni jambo
la kawaida mwanamume kurudi nyumbani akitokea kwenye majukumu yake, kumkosa
mkewe nyumbani na alikoenda kusijulikane.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles