IMESALIA wiki moja na siku chache kwa Rais Barack Obama wa Marekani. Anaondoka madarakani baada ya miaka minane ya uongozi na anakabidhi madaraka kwa hasimu wake mkubwa, Donald J. Trump.
Wakati wa kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Marekani mwaka 2008, kama ilivyokuwa kwa uchaguzi uliofanyika mwaka jana, macho na masikio ya dunia yalikuwa nchini Marekani.
Mwaka jana, dunia nzima ilikuwa ikifuatilia uchaguzi wa Marekani kutokana na wagombea wake wawili kuwa maarufu zaidi – Hillary Clinton, ambaye alitarajiwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa nchi hiyo na Donald Trump, ambaye kampeni zake zilijaa ubabe, matusi na kejeli kwa kada mbalimbali za watu.
Mwaka 2008, dunia nzima ilikuwa ikiufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Marekani kwa sababu ya mgombea mmoja tu – Seneta Barack Obama ambaye alitarajiwa kuwa Mmarekani mweusi wa kwanza kuwa Rais wa Marekani.
Hamasa yote juu ya Seneta Obama ilitokana na kumbukumbu ya Wamarekani weusi kuchukuliwa kutoka Afrika na kuuzwa huko kama watumwa, wakifanya kazi ngumu kwenye mashamba ya mabwana zao na kubaguliwa kama vile hawakuwa wakistahili kuishi kama binadamu wa kawaida.
Si hilo tu, bali hata baada ya biashara ya utumwa kupigwa marufuku, Wamarekani hawa wenye asili ya Afrika waliendelea kubaguliwa kwa kunyimwa haki za msingi, kama vile kupiga kura na kukaa kwenye kiti cha basi wakati Mzungu amesimama na kutochangamana na wazungu katika baadhi ya maeneo. Hakuna aliyewaza kwamba ipo siku, mtu mweusi atakuja kuwa Rais wa Marekani.
Pamoja na Wamarekani wapenda amani wengi kufurahia ushindi wa Seneta Obama katika uchaguzi ule, pengine Waafrika walioko Afrika walifurahishwa zaidi. Nchini Nigeria kwa mfano, walitangaza siku ya mapumziko kusherehekea ushindi wa Obama, Wakenya nao walijinadi sana kwamba anatokea kwao na hata baadhi ya Watanzania wakadai kwamba ana asili ya huku, nikimkumbuka Profesa Philemon Sarungi aliyedai kwamba Babu yake Obama anatokea huko Rorya.
Wengi wetu tulifurahishwa sana na kuchaguliwa kwa Obama kuwa Rais kutokana na Uafrika wake, asili yake. Tulichokisahau ni kwamba Obama hakuchaguliwa kuwa Rais wa Afrika, bali Rais wa Marekani, kwa ajili ya kuwatumikia Wamarekani na maslahi ya Marekani.
Tulichokisahau sisi Waafrika ni kwamba pamoja na kushangilia kwetu, bado tulitakiwa kutambua kwamba si mapenzi yetu yote yatakayotimizwa kutokana na Mwafrika mwenzetu kuchaguliwa kuongoza taifa kubwa zaidi duniani.
Tulichokisahau sisi Waafrika ni kwamba pamoja na Mwafrika mwenzetu kuchaguliwa, bado atajaribu kuendeleza tamaduni zisizo za kwetu na kujaribu kutushawishi kuzifuata ili tuwe sawa na wao, kwa kutumia kivuli cha “haki za binadamu.”
Tulichokisahau sisi Waafrika ni kwamba pamoja na Rais Obama kuwa na ngozi inayofanana na ya kwetu, haikumaanisha kwamba yeye ni sisi na haikumaanisha kwamba tukikosea basi Serikali yake haitatunyang’anya misaada, haitatuwekea vikwazo na haitatuma wajumbe kutukosoa.
Kwa kifupi, tulisahau kwamba Rais Barack Obama ni Mmarekani.
Baada ya miaka minane ya uongozi wake, natumai kwamba kila mmoja wetu atakuwa ametoka na mafunzo tofauti juu ya uongozi wa nchi na namna dunia inavyokutazama. Natumai moja ya mafunzo hayo ni kwamba Rais anapokula kiapo cha kuiongoza nchi yake, anamaanisha kuiongoza nchi yake na si kuongoza nchi zingine zisizomhusu.
Natumai jingine kati ya mafunzo hayo ni kuhakikisha kwamba unawalinda raia wenzako waliokuchagua, hata kama wakati mwingine wanafanya maamuzi ambayo yanakusononesha. Maamuzi ambayo usipokubaliana nayo, unaweza ukawa chanzo cha mgogoro ambao hautaisha katika siku za karibuni.
Haijalishi kwa kiwango gani watu wa nchi zingine wanajifananisha nawe pengine kutokana na kuzungumza lugha moja ama kufanana kwa mwonekano – kinachotiliwa mkazo ni kwamba uliapa kuilinda na kuitumikia nchi ambayo wananchi wake walikuchagua, na hivyo ndivyo unavyotakiwa kufanya.
Kwaheri Rais Obama. Binafsi nimejifunza mengi kutoka kwako.