Na Ramadhan Hassan, Dodoma
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imetaja mafanikio ambayo imeyapata katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara huku ikiahidi kuhakikisha kuwa sekta ya mifugo inaendeshwa kibiashara ili kuleta tija kwa Wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Pia imesema itahakikisha kuwa rasilimali za uvuvi zinasimamiwa ipasavyo ili kuwa na uvuvi na ukuzaji viumbe maji endelevu, maendeleo ya viwanda, ukuaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja na Pato la Taifa kwa ujumla.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Alhamisi Novemba 25,2021, Waziri wa Wizara hiyo, Mashimba Ndaki, wakati akitaja mafanikio ya Wizara hiyo amesema Wizara yake itahakikisha kuwa sekta ya mifugo inaendeshwa kibiashara ili kuleta tija kwa Wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Amesema Sekta ya Uvuvi ni mwongoni mwa sekta za uzalishaji mali ambayo ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo ya usimamizi na uratibu wa uendeshaji wa shughuli za uvuvi nchini.
“Katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara Wizara yangu itahakikisha kuwa sekta ya mifugo inaendeshwa kibiashara ili kuleta tija kwa Wafugaji na Taifa kwa ujumla,”amesema.
Aidha, Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali wa SektaBinafsi ili kukuza na kuendeleza Sekta za mifugo na uvuvi kwa kasi zaidi, chini ya uongozi mahiri wa Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia itahakikisha kuwa rasilimali za uvuvi zinasimamiwa ipasavyo ili kuwa na uvuvi na ukuzaji viumbe maji endelevu, maendeleo ya viwanda, ukuaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja na Pato la Taifa kwa ujumla.
KG 50 ZA NYAMA LITA 200 ZA MAZIWA NA SAMAKI KG 20 KWA MWAKA
Aidha,Waziri huyo amesema Watanzania wamekuwa na changamoto ya kula nyama na kunywa maziwa ambapo amedai kwa mwaka mtu mmoja anatakiwa kula nyama kg 50 na maziwa lita 200.
Aidha, kiwango cha ulaji wa samaki kwa sasa ni kilo 8.5 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na kiwango kinachopendekezwa na Shirika na Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) cha kilo 20.3 kwa mtu kwa mwaka.
MALISHO KWA WAFUGAJI
Waziri huyo amesema Serikali imetenga maeneo kwa ajili ya walisho ya wafugaji hasa katika kipindi cha kiangazi lengo likiwa ni kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.
ADAI NYAMA YA TANZANIA INA UBORA
Vilevile,Waziri Ndaki amesema nyama ya Tanzania ina ubora na ndio maana imekuwa ikinunuliwa na Nchi nyingi kutokana na ubora huo huku akiztaja Nchi ambazo zimekuwa zikinunua nyama ya Tanzania kuwa ni Oman, Kuwait, Qatar,Vietnam.
KUIMARISHA ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI
Waziri Ndaki amesema Tanzania ilianza juhudi za kulinda na kudhibiti rasilimali za uvuvi tangu ilipotunga sheria ya kwanza ya uvuvi iliyoitwa ‘Fisheries Ordinance and Trout Protection Ordinance CAP 368’.
Amesema tangu nchi yetu ipate uhuru, juhudi mbalimbali zimefanyika ili kuwezesha usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi zikiwemo kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali, kuanzisha Kanda nne (4) na vituo 35 vya doria.
BILIONI 50 UJENZI WA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO
Waziri huyo amesema Wizara inaendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kupitia Mtaalam Mwelekezi ambaye ni Kampuni ya M/S Sering Ingegneria ya Nchini Italia kwa gharama ya shilingi 1,421,041,703.
Amesema Serikali tayari imechagua eneo la Kilwa Masoko kwa ajili ya kujenga bandari ya uvuvi.
Amesema katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Bandari hiyo mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu.
Aidha, jitahada za kutafuta wawekezaji wa kujenga miundombinu mingine ya uvuvi katika eneo hilo zinaendelea vizuri.
CHANGAMOTO KATIKA UVUVI
Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) imefanya tathmini ya mahitaji ya samaki nchini ambapo makadirio ni tani 750,000 kwa mwaka ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 496,390, sawa na upungufu wa tani 253,615.
Juhudi zinazoendelea za kuongeza uzalishaji wa Samaki nchini zitaongeza ulaji wa Samaki kwa watanzania kufikia kilo 10.5 ifikapo mwaka 2026
Aidha, ili kukidhi mahitaji ya samaki nchini na kuongeza kiwango cha ulaji wa samaki, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina matarajio ya baadaye Kuimarisha miundombinu ya uvuvi kwa kujenga na kukarabati mialo, masoko na kuboresha teknolojia za uhifadhi ili kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 baada ya kuvunwa.
Pia, Kuhamasisha teknolojia sahihi za uvuvi na matumizi ya zana bora kwa wavuvi wadogo kutoka vyombo 13,593 vinavyotumia injini hadi vyombo 25,000.