29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 60 ya Uhuru| Tutaendelea kuimarisha usalama wa mipaka yetu-Dk. Tax

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, imesema itaendelea kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi inakuwa salama nakuongeza ushirikiano na wananchi katika kuibua taarifa za viashiria vya matishio ya usalama.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Novemba 29,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Stergomena Tax, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mwelekeo wa Wizara hiyo, mafanikio na changamoto katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

“Wizara itaendelea kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi inakuwa salama, pia wito wa wizara kwa wananchi ni kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa nchi kwa kujitoa kwa namna itakavyohitajika, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za viashiria vya matishio ya kiulinzi na kiusalama.

“Kama alivyowahi kusema mwasisi wa Taifa hili Hayati Mwl. Julius Nyerere nanukuu “Jukumu la Ulinzi wa Taifa ni Jukumu la kila Mwananchi” kwa muktadha huu, jukumu la ulinzi si la wizara pekee bali ni la kila mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yetu, hivyo tuendelee kuwa pamoja kulilinda taifa letu,”amesema Dk. Tax.

UKARABATI NA UJENZI WA MIUNDOMBINU

Waziri huyo amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru, serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya wanajeshi kote nchini.

“Mfano wa hivi karibuni, Wizara imetekeleza mradi wa nyumba 6,064 katika mikoa tisa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Kusini Pemba, Pwani na Tanga. Kujengwa kwa nyumba hizo kumeliwezesha Jeshi kupunguza uhaba wa nyumba za kuishi Wanajeshi na Watumishi wa Umma,”amesema.

Aidha, ukarabati wa baadhi ya nyumba za zamani pamoja na majengo ya huduma kama vile hospitali, mabwalo, mabweni ya kuishi askari, shule, vyuo na miundombinu mingine umeendelea kufanyika chini ya Wizara.

USHIRIKIANO

Amesema wizara kupitia JWTZ imeendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa(UN), Umoja wa Afrika, na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika katika Operesheni za Ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali zenye migogoro kwa kupeleka vikosi, waangalizi wa kijeshi, wanadhimu na makamanda.

Sehemu ya Waandishi wa Habari.

Amesema nchi ambazo JWTZ imewahi kushiriki katika ulinzi wa amani ni Liberia, Eritrea, Shelisheli, Ivory Coast (sasa Cote D’Ivoire), Comoros, Sierra Leone, na Sudan.

“Hivi sasa JWTZ linashiriki Ulinzi wa Amani katika nchi za Lebanon, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msumbiji na Sudan Kusini,”amesema Dk. Tax.

VIWANDA NA GAWIO KWA SERIKALI

Aidha, amefafanua zaidi kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru, serikali imeweza kuanzisha viwanda vya kijeshi ikiwemo pamoja na Tanzania Automotive Technology Centre (TATC), maarufu kama NYUMBU, Shirika la Mzinga na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT).

“Mashirika haya hufanya utafiti na uhawilishaji wa teknolojia, uzalishaji wa vitendea kazi, na bidhaa na huduma mbalimbali kwa matumizi ya kijeshi na kiraia, uzalishaji mali na miradi ya Kimkakati,”amesema.

Aidha, SUMAJKT inaendelea kujenga na kuimarisha viwanda,Kiwanda cha ushonaji Mgulani (National Service Garments Factory).

“Kiwanda hiki kimekuwa mkombozi mkubwa kwa Serikali, hususan katika vyombo vya ulinzi na usalama kwani kimeweza kushona sare mbalimbali za majeshi yetu na kupunguza gharama za ununuzi wa sare kutoka nje ya nchi,”amesema.

Amesema kuanzia mwaka wa fedha 2017/18 SUMAJKT imeweza kutoa gawio kwa Serikali la jumla ya Shilingi billioni 3.78 kutokana na faida inayopatikana katika uzalishaji.

KILIMO

Dk. Tax pia amesema wizara kupitia JKT imeendelea pia kutekeleza Mkakati wa Kilimo (2019/2020 – 2024/25) wa kuliwezesha JKT kujitosheleza kwa Chakula. Mkakati huo unatekelezwa katika vikosi vya Chita – Morogoro, Milundikwa – Rukwa, Mlale – Ruvuma, Mgambo – Tanga na Oljoro – Arusha kwa kutumia vyanzo vya ndani vya JKT, na bajeti ya Serikali.

Aidha, Wizara kupitia JKT inashiriki katika kilimo cha mazao ya kimkakati ya Taifa, ambayo ni Michikichi – Bulombora – Kigoma, Mkonge – Maramba na Mgambo Tanga, Korosho – Nachingwea na Manyoni Singida, Alizeti – Makutupora Dodoma, na Kahawa – Itende Mbeya na Tarime – Mara.

“Katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, Wizara kupitia JKT inaendelea na ujenzi wa mfumo wa umwagiliaji (irrigation scheme) katika shamba la Mpunga – Chita, ambalo ni shamba la mfano na limechangia kwa kiasi kikubwa katika kulisha vikosi vya Jeshi na kupunguza utegemezi,”amesema Dk. Tax.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles