NA FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM
MKAZI wa Mabibo, Dar es Salaam, Abraham Warioba (50), amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Sh milioni 39, baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki digidigi 20 kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Ilala, Juma Hassan, baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na mashahidi wanne wa upande wa mashtaka ambao ni Jamhuri.
Hata hivyo, Warioba ambaye ni mfanyabiashara hakuwapo mahakamani baada ya kuruka dhamana wakati shahidi wa tatu akiwasilisha ushahidi wake, hivyo ataanza kutumikia adhabu hiyo pindi atakapotiwa mbaroni.
“Mahakama inamtia hatiani mtuhumiwa kwa kumiliki digidigi 20 ambao ni nyara za Serikali, huku akiendelea kutumia vibali vilivyokwisha muda wake jambo ambalo ni kinyume cha sheria, hivyo atatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani au kulipa faini shilingi milioni 39, adhabu hii itaanza mara tu baada ya kukamatwa.
“Kwani alipo ni rahisi tu kuweza kukamatwa kwa kuwa kila kitu kipo cha kumfanya akamatwe, hivyo mahakama inatoa amri akamatwe ili iwe fundisho kwa wote wenye tabia za kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria,” alisema Hakimu Hassan.
Kesi hiyo ilikuwa na mawakili wawili wa Serikali ambao ni Florida Wenceslaus na Chesense Gavyole, ambao waliiambia mahakama hiyo kuwa hakukuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa na hivyo kuiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wote wenye tabia kama hiyo ya kumiliki nyara za Serikali bila kuwa na vibali halali.
Katika hati ya mashtaka, Warioba anadaiwa Januari 17 mwaka 2011 eneo la Pugu Kigogo Fresh, Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alikutwa akimiliki digidigi 20 wenye thamani ya Sh. milioni 3.9 ambao ni nyara za Serikali, huku vibali vyake vya kumiliki wanyama hao vikiwa vimeisha muda wake jambo ambalo ni kinyume cha sheria.