30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mhando wa Tanesco aachiwa huru

Pg 4Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, mkewe Eva Mhando na wenzao watatu, wameachiwa huru huku Jamhuri ikihusisha kuachiwa kwao na suala la rushwa.

Washtakiwa hao waliachiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, mbele ya Hakimu Mkazi Kwey Rusema ambaye hukumu aliyoandika ilisomwa na Hakimu Mkazi Hellen Riwa.

Mhando na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya   matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kujipatia Sh milioni 31.7 kwa njia ya udanganyifu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo mbali ya Mhando na mke wake, Eva Mhando, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Santa Clara Supplies, ni wahasibu wafawidhi wa Tanesco, France Mchalange, Sophia Misidai na Ofisa Ugavi, Naftali Kisinga.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Riwa alisema kwa kuangalia ushahidi uliotolewa mahakamani, suala la msingi ni mkataba kati ya Kampuni ya Santa Clara na Tanesco.

Mshtakiwa wa kwanza, Mhando, anadaiwa alishindwa kutamka masilahi yake juu ya Kampuni ya Santa Clara, kwamba inamilikiwa na mkewe Eva, hivyo kudaiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kumpa zabuni.

“Mahakama baada ya kusikiliza ushahidi ikajiuliza swali la msingi, nani anayehusika au nani alikuwa na uamuzi wa mwisho katika kutoa zabuni. Jibu ni Bodi ya Zabuni ya Tanesco, hakuna hata mshtakiwa mmoja kati ya waliopo mahakamani alikuwa mjumbe wa bodi hiyo na wala hakuna miongoni mwao aliyehudhuria mkutano uliopitisha zabuni hiyo,” alisema.

Hakimu alisema inawezekanaje mshtakiwa wa kwanza (Mhando) kueleza masilahi yake katika mkutano ambao hakuhudhuria na hakuna ushahidi kwamba aliulizwa na kutoa neno juu ya kampuni hiyo.

Kuhusu Kampuni ya Santa Clara kumilikiwa na mkewe Eva na mtoto wake, alisema jibu inawezekana Mhando asijue, kwa mazingira ya kwamba mwanamke anaweza kuwa na akaunti benki na mumewe asijue.

Hakimu alisema hakuna ushahidi wa kwamba Mhando alihusika kutumia madaraka vibaya na hakuna ushahidi wa kwamba mkewe Eva alighushi nyaraka na kuziwasilisha katika mamlaka husika.

“Kutokana ushahidi, mahakama inaona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka, hivyo inawaona washtakiwa wote hawana hatia na inawaachilia huru,” alisema.

Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, baada ya kutoka mahakamani aliweka wazi hisia zake kuhusu hukumu hiyo.

“Tunatarajia kukata rufaa, haki haijatendeka, rushwa inatisha mahakamani, ushahidi wote uliotolewa mahakamani katika hukumu wamezungumziwa washtakiwa wawili tu, Mhando na mkewe, wengine hawakuguswa kabisa, kuna haja Serikali ikaingilia kati,” alidai Swai huku akitikisa kichwa.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na jumla ya mashahidi saba na vielelezo mbalimbali.

Mhando alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka akidaiwa kuipa zabuni Kampuni ya Santa Clara Supplies Ltd, huku akijua ana masilahi nayo na kwamba anaimiliki yeye, mkewe na watoto wake.

Inadaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi na Desemba 31, mwaka 2011 katika ofisi za Makao Makuu ya Tanesco, Dar es Salaam, Mhando akiwa mwajiriwa kama Mkurugenzi wa shirika hilo, alitumia vibaya madaraka yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles