*Aitaka kuja na mpango wakujenga nyumba kwa ajili ya wastaafu
*Ahimiza ubunifu ili kujiimarisha zaidi
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
SERIKALI imeitaka Kampuni ya Nyumba ya Watumishi Housing (WHC) kuongeza ubunifu kwa kuongeza mtaji wake ili kuweza kutekeleza miradi mingi zaidiili iweze kuwasaidia Watumishi wa Umma.
Aidha, WHC imetakiwa kutanua wigo wake kwa kujikita zaidi katika maeneo ya Halmahsuri nchini ambako ndiko wanakopatikana watumishi wengi zaidi wakiwamo walimu, wahudumu wa afya, askari na wengine.
Wito huo umetolewa Jumanne Januari 18, 2021 na Waziri wa Nchi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama, alipotembelea kampuni ya Nyumba ya Watumishi Housing(WHC) kujionea miradi inayotekelezwa na kampuni hiyo ukiwamo ule wa Gezaulole uliko Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mhagama amesema lazima WHC ianze kufikiria nje ya boksi kuona ni kwa namna gani itaweza kutanua uwezo wake wa kifedha kutoka Sh bilioni 70 za sasa.
“Ni lazima tuanze kufikiri nje ya boksi, mtaji uongezeke, kuona kuna haja ya kukaa upya na bodi na sisi WHC tunahaja ya kukaa kufikiri ni kwanamna gani tunaongeza mtaji, tusisubiri mtu aje kutatua changamoto zetu kwani mahitaji ya nyumba ni makubwa,” amesema Mhagama.
Kuhusu uhaba wa nyumba kwa watumishi wa umma Magama ameielekeza WHC kushirikiana na kampuni nyingine za ujenzi ilikiwamo Halmashauri ili kukabiliana na changamoto hiyo hususan maeneo ya wilayani.
“Lakini pia nyie ndio mmeshika usukani wa ujenzi wa nyumba kwa watumishi hasa wa umma hivyo mna jukumu lakufanya hapa kuona kwamba mnaziba pengo la nyumba milioni tatu za watumishi lililopo nchini, kwani tunaelezwa kuwa kila mwaka kumekuwa na uhaba wa nyumba 200,000 za watumishi.
“Kwahiyo bodi na mifuko ya hifadhi ya jamii hebu tuzungumze tuone namna ya kulifanikisha hili, nyumba nyingi ambazo mmekuwa mkizijenga zimejengwa katika majiji makuu, lakini naomba tu niwakumbushe kwamba watumishi ambao wanamahitaji makubwa ya nyumba ni wa mikoani pamoja na wilaya na asilimia kubwa ni walimu, askari, wahudumu wa afya lakini maisha yao na makazi yao bado kuna changamoto.
“Hivyo, naomba kuagiza kwenye mipango tutakayokuja nayo sasa ikiwamo mkopo wa BoT hebu tuone namna yakuzungumza na Halmashauri za wilaya ili kuona namna ya kujenga nyumba za kuwasaidia watumishi wetu huko waliko,” amesema Mhagama na kuongeza kuwa:
“Kuna halmashauri zina viwanja hivyo tunaweza kuzungumza nao tukajenga nyumba kwa watumishi wetu hawa, hivyo CEO (Afisa Mtendaji Mkuu) naomba hili ulifikishe kwenye bodi, kwani kuna nyumba nyingi za taasisi za serikali zipo tu hazijanunuliwa mfano ikienda kule Kigamboni kuna nyumba nyingi tu, hivyo muangalia vizuri na namna ya kufikia watumishi huko waliko kwenye serikali za mitaa.
Amesema WHC inaweza pia kuangalia namna ya kushirikiana na kampuni nyingine za ujenzi ili kufanya kazi kuwa rahisi zaidi ikiwamo kushusha bei.
“Pia mjiulize je hamuwezi kushirikiana na kampuni nyingine? hivyo, mnalakujiuliza. Pia kama tunaweza kushusha bei za nyumba hizi zikaendana na mishahara ya watumishi naamini hili litakuwa jambo jema zaidi,” amesema Mhagama.
Katika hatu nyingine Waziri Mhagama ameitaka WHC kwa kushirikiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jmaii kujenga nyumba kwa watumishi ambao wamebakiza muda mfupi kazini ili wanapostaafu wawe na uhakika wa makazi bora.
“Nawapongeza pia kwa kuona umuhimu wakuanza kuuza nyumba kwa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kwani wanayo haki ya kupata nyumba. Hapa tunaweza kuangalia namna ya kuandaa nyumba kwa watumishi wanaokaribia kustaafu ili wanavyofikia muda huo wawe tayari na makazi bora,” amesema.
Awali akimkaribisha Waziri Mhagama, Afisa Mtendaji Mkuu wa WHC, Dk. Fredy Msemwa, alisema kuwa mahitaji ya makazi ni makubwa na kila mwaka kuna uhitaji wa nyumba 200,000 huku mjini kukiwa ni zaidi, hivyo wanalenga kupunguza pengo hilo lililopo.
“Jitihada za kupata ardhi kwenye mikoa mingi inaelendelea japo ardhi kwenye maeneo mengi bado haijaendelezwa, tumefanikiwa kushusha bei za nyumba ikilinganishwa na wakati ule tunaanza, kwa sasa bei zetu zina unafuu wa wastani wa asilimia 10 mpaka 30 ukilinganisha na bei ya soko.
“Pia katika kukuza mtaji tumeomba mkopo Benki Kuu kupitia Wizara ya Fedha wa Sh bilioni 20 ambao tunaamini kuwa utatuimarisha kutekeleza miradi yetu mingi,” amesema Dk. Msemwa.
Kwa mujibu wa Dk. Msemwa WHC hadi sasa imejenga nyumba 957 ambazo ziko katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Morogoro,huku kwa Dar es Salaam zikiwa Magomeni, Gezaulole na Bunju.