25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

MHADHIRI MBARONI KWA KUOMBA RUSHWA YA NGONO

NGONO

Na JONAS MUSHI-

DAR ES SALAAM

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, imemkamata Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT), Samson Mahimbo (66), alipotaka kupokea rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi wake.

Tukio hilo lilitokea juzi katika nyumba ya kulala wageni ya Camp David iliyopo Mwenge, Dar es Salaam baada ya mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) kutoa taarifa kwa Takukuru.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Dennis Manumbu, alisema awali mwanafunzi huyo alitoa taarifa ya kuombwa rushwa ya ngono na Mahimbo ili ampatie matokeo mazuri ya mtihani wa marudio (Supplementary Examination) alioufanya Januari 5, mwaka huu.

“Baada ya kupokea taarifa za mwanafunzi huyo tuliweka mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa,” alisema Manumbu.

Akieleza namna mkasa huo ulivyotokea, alisema awali kabla ya mtuhumiwa kufika katika nyumba ya kulala wageni alimtaka mwanafunzi wake afike katika Baa ya Shani iliyopo maeneo ya Sinza jirani na Baa ya Meeda ili ampatie majibu ya mtihani.

“Mtoa taarifa (mwanafunzi) alitii agizo hilo na kupatiwa majibu ya mtihani husika wa somo la road transport ambapo aliyaandika kwa dhana ya kurekebisha majibu aliyoyaandika awali.

“Baada ya kukamilisha marekebisho hayo mtuhumiwa pamoja na mtoa taarifa walielekea katika nyumba ya kulala wageni ya Camp David na kuingia katika moja ya vyumba vya nyumba hiyo.

“Wakati akiwa tayari amejiandaa kuvua nguo zote tayari kwa kuanza kutekeleza azma yake ya kumwingilia kimwili mwanafunzi huyo, ndipo maofisa wa Takukuru waliingia na kumkamata,” alisema.

Manumbu alisema uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa unaendelea kukamilishwa ili kumfikisha mahakamani.

“Natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Takukuru ili kuweza kuzuia vitendo vya rushwa na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote ambao uchunguzi utathibitisha kukabiliwa na tuhuma za rushwa ikiwamo rushwa ya ngono,” alisema.

Manumbu alisema rushwa ya ngono ni kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inayoeleza kuwa ni kosa kwa mtu kutumia mamlaka aliyonayo kumtaka mtu kimapenzi ili ampe upendeleo katika kumhudumia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles