Asha Bani, Dar es Salaam
Mwanasiasa maarufu nchini aliyekuwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Khamis Mgeja ametangaza kuachana na chama hicho na kujiunga Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Jumatano Machi 6, Mgeja amesema amejitathimini kwa kina na kwa upana ambapo ameona kwa sasa sababu zilizomfanya kuhamia Chadema hazipo.
Amesema amerudi CCM kutokana na utendaji wa Rais Dk. Magufuli kuwa mzuri na ndiyo ambao ulikuwa malengo alipokwenda Chadema awali.
“Rais Magufuli amefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuondoa rushwa, ufisadi, kuweka nidhamu ya nchi na chama na nchi kwa sasa inakwenda sawa.
“Hakuna sababu ya kubaki Chadema kwanza ni chama ambacho hawashauriki, niliwashauri waendeshe chama kisiasa lakini wamebaki wanaendesha chama kiharakati.
“Chadema ina ubinafsi mkubwa uliotamalaki wa viongozi, mfano nikiwa Ukawa, wanayo habari yao walienda kuwinda pamoja na vyama hivyo yaani NCCR-Mageuzi, NLD, CUF vilitumia nguvu kubwa kuunga mkono chadema na kuipa nguvu kubwa ya ruzuku huku vyama vingine hivi sasa haviambulii hata senti moja,” amesema Mgeja.
Mgeja aliyeambatana na familia yake alisema alitengana na familia yake kiitikadi lakini anawaomba radhi na sasa wanakwenda sawa.