30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mganga wa zahanati aliyedaiwa kubaka mwanafunzi jela miaka 30

NA MURUGWA THOMAS -TABORA

MGANGA wa zahanati aliyembaka mwanafunzi wa sekondari na kumpa ujauzito, amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Hakimu Mkazi wa Mahakama  hiyo, Jovin Kato alitoa adhabu hiyo kwa mganga huyo, Elipidius  Kweyumba ( 31), baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hakimu Kato alisema mahakama imeridhika pasipo shaka  kwamba mshtakiwa ndiye aliyembaka na kumpa ujauzito mtoto chini ya miaka 18 ambaye pia ni mwanafunzi na alifanya naye mapenzi mara nne kwa siku tofauti.

Akichambua ushahidi wa mashahidi nane wa upande wa mashtaka, hakimu Kato alisema mshtakiwa  baada ya kugundua amempa ujauzito mwanafunzi huyo, kwa kutumia utaalamu wake alimpa dawa ambazo zilimsababishia madhara.

Awali upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Tumaini Pius ulidai  mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi, mwaka huu wakati wa kipindi shule zimefungwa kupisha janga la ugonjwa wa corona.

Wakili Pius aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwa vile alitenda kosa hilo kwa makusudi ili asiweze kurudia na iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.

Akitoa adhabu hiyo, hakimu Kato aliulaumu upande wa mashtaka kwa kutokuwa makini kwani wangeweza kumwongezea shtaka la pili mshtakiwa la kusababisha mwanafunzi akose masomo.

Akitoa utetezi wake ili apunguziwe adhabu,  mshtakiwa alidai kuwa ana familia inayomtegemea wakiwemo mke, watoto na mama mzazi na kwamba mashtaka hayo ni ya kusingiziwa kwani alikuwa hajawahi kumuona binti huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles