MILAN, ITALIA
HATIMAYE mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa Argentina, Lionel Messi, juzi aliingia kwenye historia mpya ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa FIFA huku wakiwatupa nje wapinzani wake Cristiano Ronaldo na Virgil van Dijk.
Tuzo hizo zilitolewa huko Milan nchini Italia kwenye ukumbi wa Teatro alla Scala, Messi akichukuwa kwa mara ya kwanza tangu FIFA walipotengana na washirika wao French Magazine mwaka 2015. Washirika hao awali walikuwa pamoja kwa ajili ya kutoa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa Ballon d’Or, hivyo kuanzia mwaka 2016 kila mmoja alikuwa anandaa tuzo zake.
FIFA wao wakazitangaza tuzo zao zinazojulikana kwa jina la Tuzo za FIFA, wakati huo French Magazine wakibakiwa na Ballon d’Or ambazo zitafanyika Desemba 2, mwaka huu.
Hiyo ni tuzo ya kwanza kubwa kwa Messi tangu alipochukua Ballon d’Or ya tano mwaka 2015 na kuwa sawa na mpinzani wake Ronaldo.
Messi ameweza kuchukua tuzo hiyo msimu huu kutokana na kuongoza kwa kura alizopigiwa, alipata kura 46, huku Van Dijk ambaye ameshika nafasi ya pili akiwa na kura 38, huku akimuacha Ronaldo kwa kura mbili ambaye alimaliza nafasi ya tatu akiwa na kura 36.
Jambo la kushangaza ni kwamba, wachezaji hao watatu ambao waliingia katika nafasi ya mwisho ya kuwania tuzo, hakuna ambaye alijipigia kura yeye mwenyewe.
Messi aliwapigia kura wachezaji watatu ambao ni, Sadio Mane wa Liverpool na timu ya taifa Senegal, kura yake ya pili ikaenda kwa Ronaldo huku ya tatu akimpa kiungo wa kati wa Barcelona Frenkie De Jong, wakati huo Ronaldo kura zake zikienda kwa beki wa Juventus, Matthijs De Ligt, kiungo wa Barcelona, Frenkie De Jong na mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe.
Kwa upande wa Van Dijk, alimpigia kura Messi, Mohamed Salah na Sadio Mane, lakini Messi alionekana kupata kura nyingi.
Msimu uliopita Messi alimaliza huku akipachika jumla ya mabao 54, kwenye michezo 58 aliyocheza Barcelona na Argentina, akipiga pasi za mwisho 20, wakati huo Ronaldo akicheza michezo 47 na kufunga mabao 31 huku akitoa pasi za mwisho 10.