NA RAYMOND MINJA -IRINGA
MBUNGE wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), amelitaka Jeshi la Polisi mkoani hapa kuacha kufanya kazi kwa kufuata maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na badala yake wafanye kazi kwa kufuata misingi ya jeshi bila ya upendeleo.
Msigwa amesema watu wamekuwa wakionewa bila ya sababu ya msingi kwa kufuata maelekezo ya wakubwa wao badala ya kufuata sheria, weledi na misingi ya jeshi hilo.
Akizungumza na wanahabari mjini hapa jana, Msigwa, alisema wanachama na viongozi wa chama hicho wamekuwa wakikamatwa, kupigwa na kubambikiwa kesi ili kudhohofisha upinzani, jambo ambalo anasema hawatafanikiwa na wala hawatakubali kurudi nyuma.
Msigwa alisema hatakubali kukaa kimya juu ya uonevu unaoendelea mkoani hapa kwa wanachama wake kwani yuko tayari kwenda magereza bila ya kuogopa vitisho hivyo kwani wanaokwenda magereza nao pia ni binadamu kama yeye.
Alisema wanachokifanya Jeshi la Polisi cha kuwanyanyasa na kuwakandamiza wasidhani kuwa wanaibomoa Chadema bali wanaijenga kwani wananchi wanaona kinachofanywa na jeshi hilo na watawajibu.
Msigwa alisema kesi na tuhuma wanazotuhumiwa nazo ni za uongo na za kutungwa ili kuwachafua kwa wananchi.
Hata hivyo, juhudi za wanahabari zakumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julias Mjengi, ili kuzungumzia malalamiko hayo ziligonga mwamba.