Na ASHURA KAZINJA-MOROGORO
SHULE za msingi katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinafanana toka shule moja hadi nyingine.
Changamoto hizo zimesababisha wanafunzi kukosa mazingira mazuri ya kusomea na hata usalama wao kuwa mdogo au kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.
Miongoni mwa shule zinazokabiliwa na changamoto hizo ni Shule ya Msingi Matuli iliyopo katika Kijiji cha Matuli, Tarafa ya Ngerengere mkoa wa Morogoro.
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 460, wasichana 233 na wavulana 227 huku ikiwa na walimu saba tu wanaofundisha kuanzia darasa la awali mpaka la saba.
Shule hiyo inakabiliwa na tatizo la kukosa choo cha wanafunzi kutokana na choo kilichopo kukatika na kujaa hivyo kutishia usalama na afya za wanafunzi.
MWALIMU MKUU
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Edimund Milanzi, anasema hali ya choo shuleni hapo hairidhishi na kwamba hakina sifa ya kuitwa choo cha shule kutokana na kuchakaa na kuhatarisha afya za wanafunzi.
Anasema choo hicho kina matundu sita tu ambayo ni ya muda huku uhitaji ukiwa ni matundu 21.
“Hali ya choo hairidhishi kabisa, choo ni hatarishi na hakina sifa ya kuitwa choo cha shule kwa sababu kimechakaa sana na ni cha muda mrefu.
“Wanafunzi zaidi ya 460 kutumia matundu sita ni hatari, nina wasiwasi nacho hasa kipindi cha masika.
“Kiutaratibu wanafunzi wa kike 20 wanatakiwa watumie tundu moja la choo, hapa nina wanafunzi wa kike 233 hivyo yanatakiwa matundu 12. Wanafunzi wa kiume wanahitaji zaidi ya matundu tisa.
“Pia hatuna choo cha walimu, walimu tuliopo tunatumia choo kimoja ambacho nacho hakina ubora wa kuitwa choo,” anasema Milanzi.
Mwalimu huyo anaiomba serikali iangalie namna ya kuwasaidia hasa katika kutatua changamoto ya vyoo, nyumba za walimu na kero ya maji.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, nyumba za walimu zilizopo hazina hadhi kwa kuwa zimechakaa sana na kwamba kero ya maji inayowalazimu kutumia muda mrefu kutafuta maji na hivyo kukosa muda wa kufanya kazi au kupumzika na kufanya shughuli zingine.
OFISA ELIMU
Ofisa Elimu Kata ya Matuli, Joseph Chamdomo, anakiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba jitihada zinaendelea kuhakikisha kinapatikana choo kingine.
“Tatizo la choo cha wanafunzi Matuli ni la muda mrefu hata mimi nililikuta tena hali ilikuwa mbaya. Suala la chumvi liliwahi kuongelewa ni kweli lipo ila tunaendelea na jitihada za kuhakikisha choo kinajengwa kwa kutafuta wadau mbalimbali,” anasema Chamdomo.
Mwalimu huyo anasema baadhi ya wadau waliopatikana ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao wamehaidi kutoa mitambo ya kuchimbia mashimo kwa ajili ya choo hicho.
Kuhusu choo cha walimu anasema; “Mimi nilifanya jitihada fedha zikapatikana kikajengwa choo chenye matundu mawili ingawa kilijengwa chini ya kiwango.
“Aliyechukua kandarasi ya choo cha walimu alikuwa mwenyekiti wa kijiji, alipewa Sh milioni 1.4 lakini choo hakikujengwa vizuri kwa kiwango kinachotakiwa na hivyo kusabbaisha kubomoka tena,” anasema.
WAZAZI
Nao baadhi ya wanaeleza masikitiko yao kutokana na suala hilo ambalo ni hatari kwa maisha ya watoto wao huku wakishangaa uongozi husika kukaa kimya kwa muda mrefu bila jitihada za aina yoyote za kulitatua.
“Tatizo la choo hiki ni sugu na sisi tuna wasiwasi na watoto wetu, choo si rafiki kabisa na hata tukisema tuwatoe tutawapeleka wapi watoto wetu,”? anahoji Theresia Mshuza.
Mzazi mwingine, Cosmas Kidebe anasema; “Kutokana na choo hiki kuchakaa na kuwa cha muda mrefu naona si salama kabisa kwa watoto kuendelea kukitumia. Tuchukue hatua tusisubiri madhara yatokee.
MWENYEKITI WA KIJIJI, DIWANI
Akizungumzia changamoto hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Matuli, Mrisho Msonga, anasema ni muda sasa tangu choo hicho kijae na kukatika hali inayohatarisha maisha ya wanafunzi shuleni hapo.
Anasema choo hicho chenye matundu manne kinatumiwa na zaidi ya watoto 400 na kwa sasa wanafunzi wanaishi kwa kuweka chumvi ili kukifanya kinyesi kirudi chini waendelee kukitumia.
Msonga anasema kuwa mbali na kukitumia choo hicho kwa kutumia ujanja wa kuweka chumvi, lakini hali huwa mbaya zaidi hasa kipindi cha mvua.
“Choo kimejaa na mbaya zaidi kimekatika, wanafunzi wanakitumia kiujanja ujanja kwa kuweka chumvi ili walau kiwe kinanywea kidogo kuepuka kinyesi kutoka na kuzagaa.
“Imeshindikana kuifunga shule kwa sababu wanafunzi watakosa masomo,” anasema Msonga.
Naye Diwani wa Kata ya Matuli, Lucas Lemomo, anasema mvua kubwa zilizonyesha zilisababisha choo hicho kuharibika zaidi lakini kwa kushirikiana na wananchi walifanya harambee ya kuchangia fedha ili kuhakikisha choo kinajengwa.
“Choo cha wanafunzi kwa kweli ni changamoto, ilifikia hatua maofisa elimu wilaya walitaka kufunga shule kutokana na hali ilivyokuwa, hivyo tuliitisha harambee na baadhi ya wananchi walichangia lakini wengine bado” anasema Lemomo.
Anasema pia awali kulikuwa na changamoto ya choo cha walimu ambapo walilazimika kuuza bati zilizokuwa zimeezuliwa na upepo kwenye baadhi ya majengo na fedha zilizopatikana zaidi ya Sh milioni moja zilitumika kukarabati choo hicho.
“Kulikuwa na malalamiko ya choo cha walimu kilikuwa kimeboka, tulichokifanya ni kuuza baadhi ya mabati yaliyokuwa yameezuliwa kwenye baadhi ya majengo na fedha zikatumika kukarabati choo hicho ili kuondoa kero ya walimu kukosa sehemu ya kujisaidia,” anasema.
Akizungumzia sera ya elimu bure, Lemomo anasema ni shida kwani hata kuchangia choo wananchi hawataki na kuitaka halmashauri ndio ijenge choo wakiamini sera ya elimu bure inawataka wazazi kutochangia chochote na badala yake gharama zote zinabebwa na serikali.
“Ujue wananchi wanajua kwa kuwa sera ni ya elimu bure hivyo wanataka halmashauri ndio ijenge choo wakati halmashauri ina mambo mengi ya kufanya, kwakweli wananchi hawataki kuchangia kabisa hata hiyo harambee ni wachache tu waliotoa wengine mpaka leo bado” anasema Lemomo.
Akizungumzia ruzuku inayotolewa kwa ajili ya shule hiyo, anasema ni ndogo ukilinganisha na matumizi yaliyopo ambapo wanagharamia vitu vingi ikiwemo vitabu, ukarabati mdogo mdogo na kwamba kila hela inayoletwa ina matumizi yake.
OFISA AFYA
Ofisa Afya Kata ya Mkambarani, Monika Mtui, anasema kuweka chumvi kwenye choo si suluhisho na wala kitaalamu hilo halipo bali ni mbinu na mazoea yanayotutumia na jamii wakiamini inawasaidia.
“Hakuna utaalamu wa aina hiyo ni kama vile wengine wanaotumia majivu kuweka kwenye choo ili kuondoa harufu mbaya, ni mbinu ambazo watu wanazitumia wakiamini wanapunguza ukubwa wa tatitizo…ni sayansi ya kienyeji,”