Ramadhan Hassan -Dodoma
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Anthony Mavunde, amesema ajira sio kuajiriwa bali ni shughuli yoyote yenye uwezo wa kuingiza fedha.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa katika hafla ya Kampuni ya RoutePro ya kukabidhi pikipiki 30 kwa vijana wa mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Moshi, Dodoma na Singida zitakazotumika kusambaza bidhaa mbalimbali.
Mavunde alisema kumekuwa na upotoshaji mkubwa kwamba ajira ni kuajiriwa tu ofisini jambo ambalo si la kweli.
Alisema kwa mujibu wa sera ya ajira ya mwaka 2018, ajira ni shughuli yoyote inayoingiza fedha, hivyo amewataka vijana kufanya kazi na kuacha kusubiri kuajiriwa ofisini.
“Kumekuwa na upotoshaji mkubwa kwamba ajira ni kufanya kazi ofisini tu, sasa kulinagana na sera ya ajira ya mwaka 2018, ajira ni shughuli yoyote inayoingiza fedha, sasa tunahesabu leo Kampuni ya RoutePro imeongeza ajira kwa vijana wetu,” alisema.
Aliwataka vijana hao kuzitunza pikipiki ambazo wamepewa ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria za barabarani wakati wakiwa wanaendesha.
Meneja Uratibu wa Kampuni ya Route Pro, Jaja Mbazila, alisema kampuni hiyo imepata walengwa kwa kushirikiana nao kutokana na kufanya kazi katika miradi mbalimbali ya usambazaji bidhaa katika siku za nyuma.