LONDON, ENGLAND
BAADA ya timu ya Chelsea kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Cardiff City, kocha wa timu hiyo, Maurizio Sarri, amewajia juu mashabiki wanaotaka uongozi wa timu hiyo umfukuze.
Katika mchezo huo wa juzi ambao Chelsea walikuwa ugenini, kocha huyo alijikuta akiwa katika wakati mgumu kuanzia mwanzo wa mchezo, ambapo mashabiki wake walisikika wakiimba nyimba za kuuomba uongozi ufanya mpango wa kumfukuza.
Cardiff City walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 46 kupitia kwa mchezaji wake, Victor Camarasa, lakini Chelsea walifanikiwa kupata bao la kusawazisha katika dakika 84, likifungwa na Cesar Azpilicueta, kabla ya Ruben Loftus Cheek kupachika bao la ushindi dakika ya 90.
Kutokana na matokeo hayo, kocha huyo amewajia juu mashabiki hao huku akiwataka kuzomea baada ya mchezo kumalizika na kujua matokeo na si kuzomea kabla ya mchezo kumalizika kwa kuwa hauwezi kujua matokeo yatakuwaje.
“Nimekuwa nikifundisha soka kwa kipindi kurefu sasa, nimekuwa nikikutana na mashabiki wa kila aina, siku zote wamekuwa wakali hasa pale matokeo yanapokuwa mabaya.
“Lakini nawataka mashabiki wawe na utaratibu wa kuzomea mara baada ya mchezo kumalizika kwa kuwa watakuwa na matokeo sahihi, lakini watakuwa wanakosea pale wanapozomea huku mchezo ukiwa unaendelea.
“Lakini kwa upande wangu wala si tatizo kwa kuwa nimezoea hali ya mashabiki, wananifanya niwe nafikiria jinsi ya kuwatuliza,” alisema kocha huyo.
Mbali na ushindi huo wa juzi, bado Chelsea wanaendelea kushika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi, huku wakiwa na pointi 60 baada ya kucheza michezo 31, wakati huo Liverpool wakiwa vinara kwa pointi 79 baada ya kucheza michezo 32, wakati huo Man City wakiwa nafasi ya pili kwa ponti 77 baada ya kucheza michezo 31.