HATIMAYE msanii maarufu wa video za muziki wa kizazi kipya, Agnes Gerald maarufu ‘Masogange’ amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia aina mbili za dawa za kulevya, baada ya kushikiliwa na polisi kwa zaidi ya wiki moja.
Masogange amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya ikiwamo heroin mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Wilbroad Mashauri na kusomewa mashtaka mawili.
Aidha, msanii huyo ametimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 10.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 22, mwaka huu itakapotajwa tena. Masogange amefikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza baada ya jalada lake kukwama kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu mbalimbali za kisheria.