25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MASHINE HIZI KUTIKISA KAMPENI KINONDONI,SIHA

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


BAADA ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kusimamisha wagombea wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni na Siha, sasa ni wazi hamasa katika uchaguzi huo itakuwa kubwa tofauti na ule uliofanyika Januari 13, mwaka huu.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema, vinatarajiwa kutoa upinzani mkali katika kampeni zilizoanza jana, huku vikitumia viongozi wao wa kitaifa kuongoza kampeni hizo.

Kwa upande wa CCM, kinatarajiwa kuwatumia viongozi na makada wake wenye mvuto kuongoza timu ya kampeni kwa ajili ya kutafuta ushindi dhidi ya vyama vya upinzani hususan Chadema.

Makada wa CCM wanaotajwa kuongoza safu ya ‘mashambulizi’ ni pamoja na Katibu Mkuu, Abdulrahmani Kinana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Januari Makamba na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe.

Wengine katika safu hiyo, wanatajwa kuwa ni makada waliotoka Chadema akiwamo David Kafulila, Lawrance Masha na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho, Patrobas Katambi.

Timu ya Ukawa, inatarajiwa kuwajumuisha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,Katibu Mkuu, Dk. Vicent Mashinji, mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye na wabunge wote wa Chadema na CUF.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye alikiri kuwa yeye ni miongoni mwa timu kubwa na kali ambayo itaongoza kampeni katika Jimbo la Kinondoni.

Hata hivyo, Sumaye alikataa kutaja mbinu na mikakati yao ya kushinda jimbo hilo ambalo awali lilikuwa likishikiliwa na Maulid Mtulia wa CUF kabla ya kukihama chama hicho na kujiunga na CCM ambacho kimempa ridhaa ya kupeperusha bendera.

“Tumejipanga kweli kweli na kamwe hatuwezi kuanika siri na mbinu zetu za ushindi ‘unless’ unihakikishie CCM hawasomi gazeti lenu,”alisema Sumaye.

Katika uchaguzi wa marudio uliomalizika hivi karibuni katika majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea kulikuwa na hamasa ndogo pengine ni kutokana na hatua ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia uchaguzi huo.

Vyama hivyo, ni Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi. Uchaguzi uliofanyika Januari 13, mwaka huu kampeni zake zilikosa hamasa na hata idadi ya wapiga kura waliojitokeza walikuwa wachache.

Chanzo cha kususia uchaguzi huo, ni madai ya kuwapo ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za uchaguzi pamoja na matumizi makubwa ya nguvu kutoka jeshi la polisi  ambao wanashutumiwa kwamba walivuruga uchaguzi mdogo wa madiwani wa kata 43. Uamuzi wa vyama hivyo uliungwa mkono na vyama vya Chaumma na ACT-Wazalendo.

Katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Februari 17, mwaka huu katika majimbo ya Kinondoni na Siha, huenda ukaamsha hamasa mpya ya wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni na upigaji kura.

Mbali na Sumaye, wingine ambao wataongoza timu hiyo Kinondoni ni pamoja na Halima Mdee, John Mnyika, Mwita Waitara, Saed Kubenea, Maalim Seif, Julius Mtatiro, Esther Bulaya, Juma Haji Duni na Boniface Jacob.

Wengine ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Christian Mabina, Suzan Lymo, Ismael Jussa na Joseph Haule ‘profesa J’.

Kwa upande wa Siha, watakaoongoza mapambano ni Freeman Mbowe, Godbless Lema, Joshua Nassari, John Heche, John Mrema, Benson Kigaila na Ally Bananga.

Wengine ni Mchungaji Peter Msigwa, Suzan Kiwanga, Lucy Owenya, James Ole Millya, Lazaro Nyalandu, David Silinde, Pauline Gekul na Amani Golugwa.

POLEPOLE ATAMBA KUSHINDA

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alipotakiwa kutaja timu zitakazoongoza kampeni hizo, alisema kwa kawaida uchaguzi wa jimbo unasimamiwa na wilaya na mkoa husika wa chama hicho tawala.

“Hao ndio wataongoza na kuendesha mikakati, hiyo ndiyo timu yetu ya ushindi. Lakini pia watakuwepo  maofisa wachache kutoka Ofisi ndogo ya Lumumba,”alisema Polepole.

Kuhusu wabunge wengine kushiriki katika kampeni hizo, Polepole alisema wakiona inafaa watahudhuria kwenye mikutano hiyo kwa sababu uchaguzi huo ni mdogo na kwamba uchaguzi huo hauna ushindani hivyo CCM watashinda.

Uchaguzi wa majimbo hayo, unarudiwa baada ya wabunge wake, Maulid Mtulia wa Kinondoni (CUF), Dk. Godwin Mollel wa Siha (Chadema) kujivua uanachama na kujiunga na CCM kwa madai ya kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli.

Mtulia anaingia katika uchaguzi huo akikabiliwa na upinzani kutoka makundi mawili ya Chadema na CUF ambayo yalimuunga mkono katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia Ukawa na kumshinda mbunge wa siku nyingi wa jimbo hilo, Idd Azzan wa CCM.

HALI ILIVYOKUWA LONGIDO

Katika uchaguzi mdogo wa marudio uliofanyika Januari 13, mwaka huu, kampeni za Longido hazikuwa na msisimko.

Ukiachilia mbali uzinduzi wa kampeni za CCM ambao ulifanyika eneo la Longido, ndiyo ulikuwa mkutano pekee ambao ulikuwa na watu wengi lakini mingine ilidorora ikiwamo na ya vyama vya upinzani vilivyoshiriki uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Steven Kiruswa alitangazwa mshindi wa kiti hicho kwa kupata kura 41,258 ambazo ni sawa na asilimia 99.1.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Juma Mhina,ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido, alimtangaza Dk. Kiruswa kuwa mshindi wa kiti hicho kwa kupata kura 41,258.

SINGIDA KASKAZINI

Katika Jimbo la Singida Kaskazini, Justine Monko alitangazwa kuwa mshindi baada ya kupata kura 20,857 sawa na asilimia 93.5.

Katika jimbo hilo wapiga kura waliojiandikisha ni 91,518 na kura zilizopigwa zilikuwa 22,298.

Kama ilivyo katika maeneo mengine, jimbo hilo pia kulishuhudiwa na idadi ndogo ya wapigakura kwani watu 69,220 ambao ni zaidi ya asilimia 70 hawakujitokeza kupiga kura.

SONGEA MJINI

Katika uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro  wa CCM aliibuka mshindi kwa kupata kura 45,762 dhidi ya vyama vingine vya upinzani.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya aliyekuwa mbunge wake, Leonidas Gama kufariki dunia Novemba 24 mwaka jana.

Mgombea na mapingamizi

Wakati huo huo, mgombea ubunge wa Kinondoni kupitia Chadema, Salum Mwalimu amemwekea mapingamizi matano mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Maulid Mtulia.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwanasheria wa Chadema, Fredrick Kihwelo aliyataja mapingamizi hayo kuwa mgombea wa CCM kutokuwa muwazi hasa katika shughuli anazozifanya kutokana na kujaza fomu zake kuwa ni mkulima wa mbogamboga, jambo ambalo Mwalimu analipinga.

“Kajaza fomu kuwa yeye ni mkulima wa mbogamboga wakati tunajua shughuli zake je ameanza kulima mbogamboga hizo lini? Hili ni kosa kwa kuwa tayari amedanganya kisheria kwa kutoa taarifa za uongo,’’ alisema Kihwelo.

Pingamizi jingine ni uhalali wa mhuri aliotumia wa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao mwanasheria huyo alidai kuwa ni mali ya katibu na si taasisi.

“Katika hili lilitukuta mwaka 2014 wagombea wetu wa udiwani wengi takribani nusu nchi nzima walienguliwa kutokana na kutumia mhuri wa katibu na si wa taasisi, kisheria naye amekosea pia wafuate taratibu zinavyotaka,’’alisema Kihwelo.

Pingamizi jingine limetokana na madai kuwa CCM hawakutumia utaratibu wa kumpitisha mgombea huyo kwa kufuata vikao vya aina yoyote na badala yake mgombea huyo aliteuliwa juu kwa juu.

Jingine ni kutokana na madai kuwa hakufanya mrejesho wa fedha alizotumia katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015.

Fred alilitaja pingamizi jingine ni kwamba katika fomu hizo, Mtulia amekitaja chama chake cha CCM kwa kifupi badala ya kuandika Chama Cha Mapinduzi (CCM). “Na hili pia lilitukumba mwaka 2014 nusu ya wagombea wetu waliandika CDM badala ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo na hawakuruhusiwa kushiriki,’’alieleza Kihwelo.

CCM YATOA UFAFANUZI

Katibu wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Hanaf Msabaha alisema wao hawajaweka pingamizi kwa mgombea yeyote hadi jana, lakini kama Chadema wameweka wanajipanga kwa ajili ya kujibu watakapoitwa na msimamizi wa uchaguzi.

Mbali ya CCM na Chadema wagombea wengine ni Rajab Salim Jumaa (CUF), John Mboya (Demokrasia Makini) na Dk. Godfrey Malisa wa TLP.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles