Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Mashindano ya wazi ya Taifa ya kuogelea yameanza leo Septemba,23,2023, huku majaji wakitakiwa kuchagua waogeleaji mahiri wa kuunda timu ya Taifa itakayoshiriki mashindano ya Kanda, Novemba nchini Rwanda.
Jumla ya klabu 14 za Tanzania Bara na Visiwani zinashiriki mashindano hayo yanayofanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika, Masaki, Dar es Salaam.
Akifungua mashindano hayo, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Nicolas Mihayo, amesema amewaona wachezaji jinsi wanavyopambana hivyo anaamini watapata timu imara ya Taifa.
“Napenda kuwashukuru waliowezesha kuandaa mashindano haya, pamoja na waamuzi na majaji, nina uhakika mtafanya kazi nzuri bila upendeleo kama ambavyo tunaona katika michezo mingine,” ameeleza Mihayo.
Aidha amesema Serikali imesikia kilio cha wadau wa mchezo huo na watarajie kupata bwawa la kuogelea lenye vigezo vya Kimataifa mita 50/50.
Kwa upande wake Rais wa Chama Cha Kuogelea Tanzania, David Mwasyoge, amesema endapo bwawa hilo litakamilika itaongeza chachu katika kukuza mchezo huo kwa sababu wachezaji watapata sehemu bora ya kufanya mazoezi.